‘Washirikisheni walemavu kujadili mambo muhimu’

Uhuru - - Habari - NA MASANJA MABULA, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, ameishauri jamii inayoishi na watu wenye ulemavu, kuwashirikisha katika masuala ya kupanga na kutekeleza kazi za maendeleo na uchumi katika familia zao.

Amesema watu wenye ulemavu wanayo haki ya kushirikishwa katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo, hivyo siyo vyema kuwafungia ndani na kusababisha kukosa haki zao za msingi.

Ushauri huo umetolewa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa mkoa huo, Yussuf Mohammed Ali, wakati akikabidhi misaada ya mablangeti ya kuzuia mbu wa malaria, yaliotolewa na Shirika la SHINA INC, lenye makao yake nchini Marekani.

Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Kiislamu Ambasha, kilichoko wilaya ya Wete, Othman alisema serikali ya mkoa inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu na kupongeza juhudi zilizochukuliuwa na shirika hilo katika kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.

“Naiomba jamii iwe na utaratibu wa kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika kupanga, kuchagua na kutekeleza shughuli za maendeleo katika familia zao na iache tabia ya kuwafungia ndani kwani michango yao inahitajika,” alishauri.

Mapema, Rais wa shirika hilo, Jesca Kamala, alisema shirika lake limekuwa likitoa misaada kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu, ambao jamii inaonekana kuwatenga, kutowajali na kuwatelekeza.

Alisema kuwa katika kujali kundi hilo, shirika linaendelea na kazi ya kuwaendeleza kiuchumi watu wenye ulemavu, kwa kuunga mkono na kusaidia harakati za maendeleo wanazozianzisha.

Mratibu wa Shina Inc Pemba, Dadi Hamad Dadi, alisema mbali na kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, shirika hilo pia linatoa ushauri wa kitaalamu katika kuwaendeleza wajasiriamali wa kilimo cha mboga mboga na upakasaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.