CUF yafungua rasmi kesi dhidi ya msajili

Uhuru - - Habari - NA FURAHA OMARY

BODI ya Wadhamini ya Chama cha CUF, imefungua kesi rasmi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ikiiomba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, azuiliwe kuingilia masuala ya chama hicho.

Bodi hiyo ilifungua shauri hilo namba 23 la mwaka huu, huku walalamikiwa wakiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama 11 wa chama hicho.

Shauri hilo lilifunguliwa na bodi hiyo chini ya hati ya dharura kwa kupitia jopo la mawakili wao, wakiwemo Juma Nassoro, Twaha Taslima na Hashim Mzirai.

Katika shauri hilo, bodi hiyo kwa niaba ya CUF, inaiomba Mahakama Kuu mambo matatu, ambayo ni itengue barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ya Septemba 23, mwaka huu, iliyotengua uamuzi halali wa kikao cha chama.

Pia, CUF inaiomba Mahakama Kuu kumzuia Msajili asiendelee kufuatilia suala la Profesa Lipumba kufutwa uanachama.

Aidha, CUF inaomba msajili azuiwe kuingilia masuala ya chama hicho na abaki kuangalia usajili wa vyama vya siasa.

Bodi hiyo ya wadhamini imeweza kufungua shauri hilo baada ya Mahakama Kuu, kukubali maombi waliyokuwa wameyawasilisha ya kuwapa kibali cha kufungua kesi dhidi ya walalamikiwa hao.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya Mahakama Kuu, baada ya kufungua kesi hiyo, Wakili Mzirai alidai wamefungua kesi hiyo chini ya hati ya dharura ili waweze kupata udhibiti wa ofisi za chama hicho na kwa kuwa wanachama wana shauku kubwa ya kujua hatima ya chama chao.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Habari, Mawasiliano na Umma, Maharagande Mbarala, alidai mapema jana asubuhi, walikwenda ofisi za Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kufuatilia hatima ya mashitaka waliyofungua dhidi ya wafuasi wa Profesa Lipumba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.