Watatu wafariki, wawili wanusurika ajali ya mgodi

Uhuru - - Habari - NA GHATI MSAMBA, MUSOMA

WATU watatu wamefariki dunia na wengine wawili wamenusurika kufa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Katika moja ya matukio hayo, wachimbaji wadogo wa dhahabu waliangukiwa na mwamba katika mgodi mdogo wa Ekungu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Ramadhani Ngíanzi, aliwataja wachimbaji hao kuwa ni Paul Chacha (24) na Dotto Samwel (22).

Aliwataja walionusurika kuangukiwa na mwamba huo kuwa ni Masubo Masero (36) na Masumbuko Thomas (32).

Kamanda huyo alisema jana, kuwa, tukio hilo lilitokea Oktoba 17, mwaka huu, saa 5.00 asubuhi katika mgodi huo.

Ng’anzi alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mara.

Alisema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo ofisi ya kamishina wa madini kanda ya ziwa mashariki, inayohusisha mikoa ya Mara na Simiyu, bado wanaendelea na mchakato wa uchunguzi wa chanzo cha kuporomoka kwa mwamba huo unaomilikiwa na mfanyabiashara, Selestin Malundi.

Katika tukio lingine, Kamanda Ngíanzi alisema mkazi mmoja wa Kijiji cha Bujaga, Kata ya Bulinga wilayani Musoma, Robert Magesa (70), amekutwa amekufa nyumbani kwake, baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani.

Alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 17, mwaka huu, saa 4.30 asubuhi, nyumbani kwake.

Kamanda huyo alisema mwili wa Magesa umekabidhiwa kwa ndugu na jamaa kwa ajili ya utaratibu wa mazishi, baada ya kukutwa akiwa hana jeraha lolote na hakuacha ujumbe unaoeleza kujinyonga kwake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.