Madaktari bingwa wa moyo duniani walivyookoa maisha ya watoto 50

Uhuru - - Afya Na Mazingira -

ASILIMIA 33 ya watu wanaugua ugonjwa wa moyo kwa mwaka duniani. Ugonjwa huo husababisha vifo vya wagonjwa zaidi ya milioni moja huku magonjwa ya kisukari, kifua kikuu na mengineyo yasiyo ambukiza yakionyesha kupungua kwa asilimia mbili.

Kutokana na hali hiyo serikali itakuwa inaingia hasara ya dola milioni 100 kwa kuwatibu wagonjwa hao, ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa.

Inaaminika kuwa, ifikapo mwaka 2025 magonjwa yote ya moyo yatapungua kwa asilimia 25, ikiwa wananchi watapewa ufahamu wa kutosha kuhusu kuepuka na mambo yanayosababisha maradhi ya moyo.

Mambo hayo ni pamoja na vyakula, uzito, utumiaji wa dawa usiyo zingatia ushauri wa madakatari, kutokufanya mazoezi na kutokuwa na mazoea ya kupima afya mara kwa mara.

Hadi kufikia mwaka jana takwimu zinaonesha kati ya watoto milioni 1.7 wanaozaliwa nchini kwa mwaka, watoto 13,600 wanazaliwa na magojwa ya moyo. Kati yao asilimia 25 wanahitaji kufanyiwa upasuaji.

Pia gharama ya kuwasafirisha watoto kwenda Israel kupata matibabu ya moyo inagharibu sh. milioni 2.7 kwa tiketi ya mtoto mmoja tu.

Kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Ugonjwa wa Moyo Tanzania(TCS), Dk. Robert Mvungi anasema; “Elimu kwa jamii kuhusu magonjwa yasiyoambukizwa ni lazima ipewe kipaumbele ukiwemo ugonjwa wa moyo ambao umeonekana kuongezeka kwa kasi na kusababisha vifo vingi nchini,”

Anasema asilimia 80 ya ugonjwa huo unaweza kupungua endapo wananchi watafuata vigezo vya kujiepusha nao ikiwemo kufanya mazoezi, kutokuvuta sigara, na kuacha kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi.

Katika kuendeleza mapambano dhidi ya maradhi ya moyo, Oktoba, 8 hadi 15 mwaka huu, Tanzania ilipata bahati ya kutembelewa na jopo la madakatari bingwa wa moyo duniani.

Jumla ya madakatari hao ilikuwa ni 35, ambao waligawanyika katika makundi matatu, ambayo ni madakatari bingwa wa upasuaji wa moyo, madakatari bingwa wa kuziba matundu katika moyo bila kupasua na wataalam wa dawa.

Jopo hili liliungana na madakatari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, ambapo kwa pamoja waliendesha kambi ya matibabu ya moyo bure kwa watoto.

Kambi hiyo, iliandaliwa na taasisi ya kidini ya Dhi- Nureyn Islamic Foundation (DIF), yenye makao makuu yake mkoani Iringa , kwa kushirikiana na taasisi ya Muntada Aid ya Uingereza na JKCI.

Katika kambi hiyo, watoto 50 wamepata matibabu ya moyo bure.

Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo, Katibu Mkuu wa DIF, Dk. Shamsi Elmi, anasema, lengo la kambi hiyo lilikuwa ni kuwafikia watoto 70 hadi 80 waliokuwa wanaugua maradhi ya moyo.

Anasema, kati ya hao 50 watoto 24 walipata matibabu ya kiwango cha juu ya kuzibwa matundu katika miyo yao.

“Watoto 26 walifanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo ‘Open Heart’,” anaeleza Dk. Elmi.

Anadai; “Upasuaji huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa ya asilimia 100, kwani hakukuwa na mtoto aliyepoteza maisha,”

“Kwa kuwa lengo la kambi yetu lilikuwa ni kutibu watoto 70 hadi 80, hivyo kufikia wagonjwa 50 ni mafanikio makubwa,”alisema Dk. Elmi.

Madaktari hao bingwa waligawinyika na kwenda katika Hospitali ya Mnazimmoja, Zanzibar, ambako ndani ya siku moja tu walibaini watoto 66 waliokuwa na maradhi ya moyo.

Dk. Elmi anasema , hii ni kambi ya tatu kwa madakatari bingwa wa moyo duniani , kukusanyika hapa nchini kwa ajili ya kufanya upasuaji bure kwa watoto.

“Mei 2015, DIF kwa kushirikiana na Taasisi ya Muntada Aid ya uingereza ziliandaa kambi ya matibabu ya moyo kwa watoto wenye matatizo ya moyo ambapo jumla ya wagonjwa 66 walipata matibabu, ikiwa ni pamoja na upasuaji na uzibaji wa matundu katika moyo,“

“Katika kambi ya Mei 2016 wagonjwa 75 wameweza kufaidika na kambi kama hiyo,“anaeleza Dk. Elmi.

Hata hivyo Dk. Elmi anadai, changamoto kubwa inayojitokeza katika kambi hizo ni watu wa mikoani kushindwa kuwafikisha watoto katika kambi kutokana na gharama.

“Tunatoa wito kwa wafanyabishara na mashirika ya misaada kutuunga mkono katika kambi zijazo kwa kudhamini gharama za nauli za fedha za kujikimu kwa familia zinazotoka nje ya Mkoa wa Dar es salaam,”alieleza katibu huyo.

Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, aliipongeza DIF, Taasisi ya Muntada Aid ya Uingereza na madakatari wote waliofanikisha matibabu hayo.

“Matibabu ya moyo ni ghari hivyo wananchi wengi wanashindwa kumudu . Tunaamini kwamba kufanikisha matibabu ya watoto 50 bila malipo ni hatua kubwa ,”anasema Profesa Janabi.

Anasema, JKCI imejidhatiti vya kutosha katika kutoa matibabu ya moyo kwa kiwango hususan katika upasuaji na kutibu moyo bila kupasua pamoja na uzibaji wa matundu ndanani ya moyo.

Anasema hospitali hiyo tayari imewafanyia upasuaji zaidi ya watoto 600 kuanzia mwaka jana hadi sasa.

“Taasisi imewekeza zaidi katika kununua vifaa tiba vya kisasa na kuwawezesha madaktari na wauguzi kupata mafunzo kutoka nje ya nchi,” ameeleza

Amesema JKCI imekuwa upasuaji kwa zaidi ya asilimia 90.

Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji ikifanikisha (JKCI) ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji moyo, Bashir Nyangasa, anadai kuwa ujio wa madakatari bingwa kutoka nchi mbalimbali duniani, ilikuwa ni fursa ya kipekee katika kufanikisha kazi hiyo.

“Wametusaidia vifaa vya kisasa vya kufanikisha upasuaji huo lakini pia na kutongezea ufahamu zaidi juu ya masuala ya moyo.

Unapozungumzia kutibu watoto 50 maradhi ya moyo, inaweza kuonekana ni idadi ndogo, lakini kwa jinsi matibabu hayo yalivyo na yanavyifanyika hiki ni kiwango kikubwa ambacho tunaamini kinatufanya tujivunie mafanikio hayo,”anaeleza Dk. Nyangasa.

Anaongeza; “Matibabu hayo yalitolewa bure bila mgonjwa kutozwa hata senti moja, hivyo yameweza sit u kuokoa uhai wawatoto 50 bali pia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho wazazi au walezi wangetoa ama serikali kugharamia matibabu yao,”

“Tunaamini, uhusiano baina ya KJCI , DIF na Muntada Aid, utadumishwa ili tuwe na kambi za mara kwa mara kama hizi kwa ajili ya kupambana na maradhi ya moyo ambayo ni miongoni mwa maradhi hatari duniani yanayo poteza maisha ya watu wengi wakiwemo watoto,”anasema Dk. Nyangasa.

Akizungumza kwa niaba ya jopo la madaktari kutoka nje ya nchi,kiongozi wa msafara wa madakatari hao Dk. Loay Abdulsamd, anaeleza kwamba licha ya matibabu hayo kuwa ya kiwango cha juu yamefanyika kwa ufanisi mkubwa.

“Tanzania ina watoto wengi wenye matatizo ya moyo, hivyo tunaamini tunalojukumu kubwa katika kulishughulikia tatizo hilo. Kambi hii ni kwa ajili ya kujitolea. Ni kazi inayohitaji moyo wa kizalendo na,”alisema Abdulsamd.

Anaongeza; “Kambi ya moyo ya madakatari wa Muntada Aid ndiyo kambi kubwa zaidi duniani ukilinganisha na kambi za taasisi zingine kwa wingi wa madakatari bingwa na waliobobea katika masuala ya moyo.

“Hii ni fahari kwa Tanzania, kufanikisha kambi hii. Lakini tunaamini haitaishia hapa, Tutaendelea ili tuweze kuwafikia watoto wengi zaidi wanaosumbuliwa na mardhi hayo hatari,” anabainisha Dk. Abdulsamd.

MKURUGENZI wa Huduma za Upasuaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),Dk. Bashir Nyangasa(katikati),akiongeanawaandishiwahabari,kuhusukambi ya matibabu ya moyo bure kwa watoto iliyoandaliwa na taasisi ya Dhi Nureyn Islamic Foundation (DIF), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hivi karibuni. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Shams Elmi na kulia ni Dk. Loay Abdulsamd, mwakilishi wa madaktari bingwa wa moyo.

RAIS Mstaafu Dk.Jakaya Kikwete akimjulia hali mtoto Habiba Lipande(6) ambaye alifanyiwa tiba ya kuziba tundu lililokuwa katika moyo kwa kutumia teknolojia mpya bila upasuaji wa kifua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili hivi karibuni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.