Uhaba wa ardhi Geita changamoto inayochangia uharibifuwa mazingira

Uhuru - - Afya Na Mazingira - NA MWANDISHI WETU

IFADHI za misitu ni rasilimali muhimu kwa taifa, mataifa mengi duniani ikiwemo Tanzania yamekuwa mstari wa mbele kupiga vita uharibifu wa hifadhi za misitu na wanyamapori kwa mustakabali wa taifa. Takwimu zinaonyesha kwa sasa Tanzania inapoteza takribani hekta 372, 000 za uoto wa asili kila mwaka na kama kasi hiyo ikiachwa iendelee tishio la kutoweka kwa uoto huo ni mkubwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, inaonyesha kuwa Tanzania ina eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa takribani hekta milioni 48.1 na kwamba kasi iliyopo ya uharibifu ikiachiwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129.

Kutokana na hilo serikali imekuwa mstari wa mbele kuwakumbusha wananchi wote wajibu wao kutii sheria na kuepuka vitendo viovu vinavyosababisha kupotea kwa uoto wa asili kwa kasi inayoendelea hivi sasa na nchini na kutishia uhifadhi endelevu.

Hali hiyo itasababisha nchi kuwa jangwa kutokana na ukataji wa miti hovyo, kilimo kisicho endelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji makazi na shughuli zingine za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwa ni hifadhi za misitu, mapori ya akiba, mapori tengefu na hifadhi za taifa.

Kutokana na kuzingatia tishio hilo na umuhimu wa hifadhi katika taifa kiuchumi, kijamii na kiikolojia, serikali ilitunga sera, sheria, kanuni na taratibu kwa madhumuni hayo.

Sheria hizo ni pamoja ya uhifadhi wanyamapori, Na.5 ya mwaka 2009, sheria ya misitu Na.14 ya mwaka 2002, sheria ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, sura 284, R.E 2002 na sheria ya hifadhi za taifa, sura 282, R.E 2002.

Viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na viongozi wengine wamekuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu na wanyamapori kutii sheria za uhifadhi na kujiepusha na vitendo viovu vya uharibifu wa mazingira.

Inaelezwa kwamba vitendo hivyo vinapelekea kupotea kwa uoto wa asili na kutishia nchi kuwa jangwa ambapo pamoja na mambo mengine,wananchi wanatakiwa kuondoa mifugo yao katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Geita, aliwataka viongozi na watendaji wa mkoa huo kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo ya hifadhi mkoani huo na taifa kwa ujumla.

Mhandisi Makani alitoa maelekezo hayo akiwa katika wilaya ya Chato, ambapo alivitaja vitendo vya uharibifu wa mazingira kuwa ni ukataji wa miti hovyo, kilimo kisicho endelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji makazi na shughuli zingine za kibinadamu.

Anasema shughuli hizo zote zinafanywa katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwemo hifadhi za misitu, mapori ya akiba, mapori tengefu na hifadhi za taifa.

“Kwa sasa Tanzania, inapoteza takriban hekta 372,000 za uoto wa asili kila mwaka, endapo hali hiyo ikiachwa iendelee tishio la kutoweka kwa uoto huo ni kubwa zaidi,” anasema.

Mhandisi Makani anaongeza kuwa takwimu pia zinaonyesha kuwa Tanzania ina eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa takriban hekta milioni 48.1 na iwapo kasi hiyo ikiachwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129.

Kuhusu utaratibu wa kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria, Mhandisi Makani anasema watumishi na viongozi wa serikali wanaotekeleza zoezi hilo wanatakiwa kufuata sheria na miongozo iliyowekwa.

Anataja miongozo hiyo kuwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo viovu vinavyoweza kuichafua serikali ikiwemo rushwa na unyanyasaji wa wananchi na kwamba watakaobainika kwenda kinyume na utaratibu huo watachukuliwa hatua za kisheria.

Naibu Waziri huyo aliwataka watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia sheria hizo kila siku na kuendesha utekelezaji wake kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mikoa ili kuimarisha utekelezaji wa sheria hizo na kuweka uwazi katika utendaji.

Aliwataka wananchi waliopo katika vijiji na vitongoji vilivyosajiliwa kisheria kutoanzisha au kuendeleza shughuli mpya za kibinadamu hususan zinazosababisha uharibifu wa mazingira ikiwemo kuathiri mabadiliko ya tabia nchi.

Anasema kwa sasa wananchi hao wanatakiwa kusubiri kikosi kazi cha kitaifa kitakapokamilisha kazi yake na kuishauri serikali namna bora ya kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Tayari serikali imeunda kikosi kazi maalumu cha wataalamu chenye wajumbe kutoka wizara sita ambazo zinahusika moja kwa moja na changamoto mbalimbali za ardhi.

Lengo la kikosi kazi hicho ni kufanya uchunguzi wa kina ikiwemo kupitia sheria zote zinazohusika kabla ya kuishauri serikali namna bora ya kumaliza migogoro ya ardhi ikiwemo kwenye maeneo ya hifadhi.

Mhandisi Makani anazitaja wizara zinazounda kikosi kazi hicho kuwa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii, TAMISEMI na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo ndizo zimeanza utekelezaji wa zoezi hilo linalotarajiwa kukamilika mwezi Desemba, mwaka huu.

Hata hivyo anasema wizara nyingine mbili zitaungana baadae kukamilisha zoezi hilo ambazo ni maji na umwagiliaji na nishati na madini.

“Sitaraji kuwa wananchi wengine watatumia vibaya tamko hili na kuanza kuingia katika maeneo ya hifadhi kwa shughuli zozote zile za kibinadamu kwani vitendo hivyo havihusiani na tamko hili na hatua kali zitachukuliwa mara moja dhidi ya wale watakao kwenda kinyume,” anasema.

Lakini Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga, anasema mkoa huo unakabiliwa na uhaba wa ardhi uliosababishwa na ongezeko kubwa la watu waliovutiwa na shughuli za uchimbaji wa madini, uvuvi, ufugaji na kilimo.

Anasema shughuli hizo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa ni changamoto kubwa katika uhifadhi mkoani humo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe, anasema kumekuwepo na uharibifu wa misitu wilayani humo ambapo Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo Kahama imeharibiwa kwa asilimia 70 kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na makazi ya kudumu hali inayohatarisha kutoweka kwa hifadhi hiyo.

Msitu wa Biharamulo-Kahama una ukubwa wa hekta 134,684 na upo katika wilaya za Chato, Bukombe na Biharamulo ambpo kwa upande wa Chato umeharibiwa kwa asilimia 70.

Inaelezwa kwamba msitu huo una ukubwa wa eneo la hekta 30,000.

NAIBU Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama uliopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita, hivi karibuni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.