TPB yatatua tatizo la uhaba wa vyoo Kyela

Uhuru - - Afya Na Mazingira - NA MWANDISHI WETU

BENKI ya Posta Tanzania (TPB), imetoa msaada wa jengo la choo lenye matundu matano katika shule ya msingi Ipinda, iliyoko wilayani Kyela, mkoani Mbeya.

Jengo hilo lina thamani ya sh. milioni tisa, ambapo kati ya matundu hayo matano, mawili ya walimu wa kiume na moja kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa miguu.

Meneja Mwandamizi Uhusiano wa Umma wa TPB, Noves Mosses, alisema hayo jana, wakati akikabidhi jengo hilo kwa uongozi wa shule hiyo.

Alisema wameamua kutoa msaada huo baada ya kupokea maombi kutoka kwa kamati ya shule hiyo kuhusu kutokuwepo kwa vyoo bora na salama vya walimu.

Mosses alisema shule hiyo haikuwa na choo kitakachoweza kutumiwa na walemavu, badala yake walilazimika kutumia vyoo vya kawaida ambavyo vilikuwa vinawapa wakati mgumu kutokana na miundombinu yake kutokidhi mahitaji yao.

Alisema mara nyingi wadau wa elimu huangalia mahitaji ya wanafunzi na kuwasahau walimu, ambao wana changamoto katika mazingira yao ya kazi, yanayosababisha kushindwa kutoa elimu kama inavyostahili.

“Tumeamua kutoa msaada huu baada ya kuguswa na uhaba wa vyoo katika shule hii, kwani watoto hawa ni watoto wetu sote na ni jukumu letu kama wazazi kuona umuhimu wa jambo hili na kuwasaidia,”alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Takwimu na Vifaa katika Ofisi ya Elimu Wilaya ya Kyela, Lusian Kavishe, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alisema msaada huo ni mkubwa katika shule hiyo kwani haikuwa na uwezo wa kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo hilo.

Alisema jambo lililofanywa na TPB ni kubwa na ni mfano wa kuigwa katika jamii na kuzitaka taasisi na kampuni zingine, kujitokeza kusaidia ujenzi wa vyoo ndani ya wilaya ya Kyela na jiji la Mbeya.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Subira Gwakabale, aliishukuru Benki ya Posta kwa msaada huo kwani haikuwa rahisi wao kutekeleza ujenzi wa vyoo hivyo.

“Tunaishukuru Benki ya Posta kwa msaada huu, kwani muda mwingine ilikuwa inatulazimu kwenda kuomba msaada kwenye nyumba zilizopo jirani na shuleni kwetu”, alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.