SOS kuzindua kijiji kipya cha watoto Mwanza

Uhuru - - Afya Na Mazingira - NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la SOS, linatarajia kuzindua kijiji kipya cha watoto katika maeneo ya Bugarika, mkoani Mwanza.

Kijiji hicho kipya kitawapa watoto fursa ya kujenga uhusiano wa kifamilia ulio imara, ambapo kila mtoto atapata mama wa kumtunza na atakuwa na kaka na dada zake katika mazingira ya kijiji.

Mkurugenzi Mkuu wa Taifa wa SOS Chidrenís Villages Tanzania, Anatoli Rugayemukamu, kupitia taarifa kwa waandishi wa habari, alisema kijiji hicho kimegharimu Dola za Kimarekani milioni 4.4.

Alisema kijiji hicho kina nyumba 12, zenye uwezo wa kuhifadhi watoto 120, jengo la utawala, shule za chekechea na nyumba ya wageni.

“Mradi huu pia umehusisha ukarabati wa shule ya msingi ya Igegeleo ili kuhakikisha wote wanapata elimu bora ya msingi,” alisema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, uzinduzi huo utafanyika Oktoba 25, mwaka huu na kuhudhuriwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

“Kama shirika, tunaamini kuwa kila mtoto ana familia na anatakiwa kupata upendo katika makuzi yake, heshima na ulinzi na ndio maana tukaamua kutoa malezi ya aina hii ya kifamilia kwa watoto yatima na ambao wametelekezwa na wazazi wao.

“Kwa malezi ya familia tunayotoa hapa, watoto wanapata malezi bora na kutokana na nyumba zao kuwa pamoja na karibu, tunakiita kijiji cha SOS,”alisema.

Alisema shirika hilo liliasisiwa na Herman Gmeiner kutoka Tyrol, Austria, mwaka 1949, baada ya kuguswa na namna watoto wanavyopata na shida baada ya vita ya pili ya dunia.

Alisema SOS Childrenís Village inafanya kazi katika nchi 134 na inasaidia maelfu ya watoto kupitia mpango wa malezi na kuimarisha familia na namna nyingine za kijamii.

Rugayemukamu alisema SOS imekuwa ikifanya kazi nchini tangu mwaka 1991, na inavyo vijiji katika miji ya Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na imehakikisha kuwa watoto wanapata malezi bora ya kifamilia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.