Jaffo awataka viongozi kufanyakazi kwa ufanisi

Uhuru - - Afya Na Mazingira - NA ALLAN NTANA, TABORA

WATUMISHI wa umma wametakiwa kutumia vizuri taaluma zao sambamba na kuongeza ufanisi wa kazi ili kuleta tija kwa manufaa ya wananchi wanaowatumikia.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jaffo, alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega na Nzega Mji.

Alisema watumishi wa umma wakitumia elimu na taaluma zao vizuri, utumishi wao utakuwa na tija kubwa katika halmashauri na ufanisi utaongezeka zaidi tofauti na hali ilivyo kwa sasa.

Jaffo alisema kwa kutumia taaluma zao, ni vema watumishi hao wakafanya kazi kwa moyo wa kujiamini na kushirikiana vyema ili kutimiza azma ya serikali ya awamu ya yano ya ‘Hapa Kazi Tu’.

Naibu waziri aliwataka wakurugenzi, maofisa utumishi na wakuu wa idara katika halmshauri hizo mbili, kutopendelea au kuwagawa, bali wajikite katika kutambua ufanisi na kutoa fursa sawa kwa kila mtumishi.

Mbali na mambo mengine, Jaffo alitembelea mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya sekondari ya Bulunde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupula, alisema tatizo kubwa linaloathiri ufanisi wa watumishi walio wengi katika halmashauri ni kutojiamini na hivyo kutekeleza majukumu yao kwa woga.

“Naamini kila mtumishi akijiamini na kutumia vizuri taaluma au elimu yake ya shahada ya kwanza au ya pili, hakuna mtu atakayewagusa au kuwasema vibaya kwani kila mfanyacho kitakuwa katika mstari ulionyooka,” alisema.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussen Bashe, aliishukuru serikali kwa kuanza kutimiza ahadi yake ya kutatua kero ya maji kwani zaidi ya sh.milioni 400, zimetolewa kutekeleza mradi wa maji.

Aidha, alimshukuru naibu waziri kwa kukubali kutembelea wilaya hiyo na kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.