‘Rushwa, dawa za kulevya bado tatizo kwa wananchi’

Uhuru - - Afya Na Mazingira - NA DUSTAN NDUNGURU, SONGEA

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, amewataka Watanzania kushirikiana na serikali katika kukabiliana na maadui wanaohatarisha maendeleo.

Amewataja maadui hao kuwa ni rushwa, dawa za kulevya, ukimwi na malaria, ili hatimaye juhudi zinazoendelea za kuondokana na umasikini ziweze kufanikiwa.

Oddo alitoa mwito huo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

Alisema maadui hao wamekuwa kikwazo kikubwa nchini katika sekta mbalimbali na kwamba, iwapo wataendelea kushika hatamu, taifa litashindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mwenyekiti huyo alisema rushwa haipaswi kupewa nafasi kwani imekuwa ikisababisha wanyonge kukosa haki zao za msingi na wananchi kulalamika.

“Wananchi kamwe wasikubali kutoa rushwa pindi wanapokwenda katika ofisi mbalimbali za serikali ili kupata huduma.

“Pale ambapo watakutana na adha hii, wasisite kutoa taarifa kwa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambao wapo katika kila wilaya nchini,”alisema.

Oddo alisema juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano za kupambana na wala rushwa na mafisadi, iwapo zitafanikiwa, zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuondosha malalamiko kwa wananchi.

Akizungumzia dawa za kulevya, Oddo alisema wazazi wana kila sababu ya kuwaelimisha vijana wao wasijihusishe na dawa hizo kwa kuwa madhara yake ni makubwa katika jamii.

Aidha, Oddo aliwataka Watanzania kwenda katika vituo vya afya kupima afya zao ili waweze kufahamu kama wameambukizi maradhi ya ukimwi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.