Madaktari bingwa wa MOI wawasili Tabora

Uhuru - - Habari - Na Allan Ntana, Tabora

TIMU ya Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Muhimbili Orthopaedic Institute (MOI), wamewasili mkoani Tabora kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya upasuaji kwa watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Akitoa taarifa jana, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Elisha Ndakama, alisema maandalizi yote yamekamilika na hadi sasa watoto 15, watano wa kike na 10 wa kiume 10, wameandikishwa kwa ajili ya kufanyiwa operesheni hiyo.

Akizindua zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, aliishukuru Kampuni ya GSM Foundation ya jijini Dar es Salaam, kwa uamuzi wao wa kufadhili zoezi hilo kwa ushirikiano na MOI, ambayo imetoa madaktari bingwa wa kuendesha upasuaji huo.

Mwanry alisema mkoa wake unahitaji sana huduma hiyo na wamehamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi na kuleta watoto au ndugu zao wenye matatizo hayo.

Aidha, alisema wameweka mazingira wezeshi kwa madaktari hao ili kufanikisha zoezi hilo katika muda uliopangwa.

Mkuu huyo wa mkoa alisema akiwa mlezi wa watoto, kinamama na wazee wa mkoa huo, anajisikia faraja kubwa kutokana na ujio wa madaktari hao.

Kiongozi wa madaktari hao, Dk. Hamis Shaban, alisema msafara wake umewasili Tabora ukiwa na daktari bingwa mmoja, madaktari wasaidizi watatu, mtaalamu wa dawa za usingizi mmoja na wauguzi watatu.

Alisema kutokana na vifaa vya kisasa walivyonavyo pamoja na wataalamu hao wenye uzoefu, wana uwezo wa kuwafanyia upasuaji watoto 20 kwa siku.

Alimuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa, kwa siku tatu watakazotoa huduma mkoani humo, wataweza kuwahudumia watoto 60 na wako tayari kufanya kazi usiku na mchana.

Alisema hadi sasa zaidi ya watoto 199, wameshafanyiwa upasuaji huo kwa mafanikio makubwa, hivyo aliwataka wakazi wa Tabora wenye watoto au ndugu zao, wanaokabiliwa na tatizo la kichwa kikubwa au mgongo wazi, kuwaleta kwa wingi ili wapatiwe huduma hiyo.

Ofisa Habari wa GSM Foundation, Khalfan Kiwamba, alisema zoezi hilo ni endelevu na litachukua takribani miezi mitatu au minne mpaka kukamilika kwake, na litafanyika katika mikoa yote ya Tanzania.

Alisema hadi sasa wametoa huduma hiyo katika mikoa 14.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.