Viongozi CCM watakiwa kuacha upambe

Uhuru - - Habari - NA BLANDINA ARISTIDES, MWANZA

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela, Nelson Meshack, amewataka viongozi wa Chama kujenga mazoea ya kuhudhuria vikao vya kikatiba mara kwa mara kwa lengo la kujifunza zaidi.

Pia, amewaasa viongozi hao kuacha kuwa wapambe katika Chama, badala yake wafanye kazi ya kukiimarisha na kujenga umoja na mshikamano kati yao.

Akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya, juzi, Meshack alisema kazi ya kuimarisha Chama haihitaji kufanywa kimchezomchezo, badala yake ifanyike kwa kutumia vikao maalumu na walengwa wahudhurie bila kukosa.

“Tuache uvivu wa kuhudhulia semina na vikao vya Chama. Najua wapo watu baada ya kutolewa agizo la kutofanyika kikao chochote cha siasa, walishangilia na walinenepa. Lakini kwa wanaofahamu umuhimu wa vikao, bila shaka walikonda,” alisema.

Aliongeza kuwa ni vema viongozi hao wakatambua umuhimu wa vikao badala ya kukaa bila kujua Chama kinaendeleaje na nini kinafanyika.

Alisema kukosekana kwa semina na vikao katika ngazi zote za Chama ni sawa na askari aliyeko vitani bila kuwa na silaha.

Meshack alisema wapo baadhi ya wana-CCM, ambao wamekuwa wapambe wa Chama, kutokana na matendo yao kuweka mbele zaidi maslahi binafsi.

Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa aina hiyo hawatakiwi katika Chama kwani ni waporoshaji na wanajali zaidi maslahi yao.

“Mtu akiona uchaguzi umekaribia, anaanza kugawa kadi kwa watu hata ambao hawana mapenzi na Chama, ilimradi apewe uongozi. Hali hii ni ya kukemea mapema,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.