Wanasiasa ndio chanzo

Watajwa kuitumia kwa manufaa yao ya kisiasa Kamati ya bunge yataka kuzikutanisha wizara tano

Uhuru - - Mbele - NA WILLIAM SHECHAMBO, DODOMA

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo na Ufugaji, wamesema chanzo kikuu cha migogoro ya wakulima na wafugaji nchini ni wanasiasa.

Aidha, wamekubaliana kumuita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili asikilize mapendekezo yao yenye lengo la kukomesha tatizo hilo sugu nchini.

Wamesema kwa muda mrefu migogoro ya makundi hayo imeshindwa kutatuliwa na kusababisha mamia ya Watanzania kupoteza maisha na mali zao, hivyo lazima kutafutwe suluhisho la kudumu.

Kamati hiyo ilifikia maamuzi hayo katika kikao kilichofanyika jana, mjini Dodoma, kati yao na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Kilimo na Mifugo, akiwemo Waziri wa wizara hiyo, Dk. Charles Tizeba.

Walisema kuna umuhimu Waziri Mkuu kutoa ruhusa kwa kamati hiyo kuwakutanisha mawaziri watano, ambao wizara zao zinahusika kwa namna moja au nyingine kwenye migogoro hiyo.

Mawaziri hao ni kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Maliasili na Utalii; Wizara ya Maji na Umwagiliaji; TAMISEMI; Viwanda na Biashara na Mambo ya Ndani.

“Hatuwezi kumaliza hili tatizo kwa kukutana hapa na Dk. Tizeba na wenzake wachache, tunahitaji mawaziri watano kama sio sita, ili tumalize kabisa tatizo hili,” alisema Philip Mulugo, ambaye ni mmoja wa wajumbe.

Mbele ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mary Nagu, wajumbe hao walisema wanasiasa bila kujali itikadi za vyama vyao ndio chanzo kikuu cha migogoro kutokana na kuwanufaisha kisiasa.

“Wanasiasa sisi wenyewe ni chanzo cha tatizo hili, tukiona wakati huu wakulima watatusaidia kupata kura nyingi, tunawaunga mkono, tukiona sasa ni wafugaji, tunawatetea, hili ni tatizo,” alisema Mahamoud Mgimwa, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Pia, alisema lawama zinaelekezwa kwa wananchi kutokana na akili yao ya kucheza na vichwa vya wanasiasa, ambapo wanajua fika kuwa mwanasiasa atawaunga mkono hata kama hawako sahihi kutokana na kiu yake ya kura.

Mgimwa alisema kuna tatizo kubwa kwenye uhusiano baina ya wizara, ambapo licha ya kuwepo kwa ranchi nyingi nchini, bado hazijaweza kutumiwa vizuri kutatua changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji.

Alisema wakati serikali ikiwashauri wafugaji kupunguza idadi ya mifugo yao na kuanza kufuga kisasa, ilitakiwa ranchi zitumie fursa hiyo kukusanya mifugo mingi yenye viwango ili kuisafirisha nje ya nchi kwenye soko la nyama.

“Kwa taarifa, Tanzania ni ya pili kwa kuwa na ng’ombe wengi Afrika baada ya Ethiopia, hivyo tuitumie fursa hii kutatua tatizo hili, soko lipo kubwa tu nchi za Uarabuni,” alisema.

Kwa upande wake, Pascal Haonga, aliunga mkono hoja ya Mgimwa, kwa kusema kuwa, licha ya kwamba Tanzania inaelezwa kuwa ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe Afrika, inatakiwa kuchangia ukuaji wa pato la taifa, badala ya kusababisha matatizo.

Awali, Waziri Dk. Tizeba, aliwasilisha mbele ya kamati hiyo, taarifa ya mipango ya wizara yake kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, ambapo alibainisha maeneo yenye tatizo hilo nchi nzima, ikiwemo wilaya za Kilosa, Kiteto na Kongwa.

Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, akizungumza kuhusu taarifa hiyo, alisema ina mapungufu, hususan kwenye kubainisha maeneo yenye mgogoro, ambapo kwa mkoa wa Pwani, maeneo lukuki yaliyotajwa katika wilaya ya Mkuranga, hayana matatizo hayo.

“Ninawashauri watu wa wizara, kaeni chini mbainishe tena maeneo yenye matatizo ya wakulima na wafugaji kwa sababu kwa taarifa yenu maeneo yote ya wilaya ya Mkuranga mliyoyataja, hayana shida hiyo, sana sana ni matatizo ya mipaka ya wawekezaji,” alisema.

Alisema ni vizuri wizara hiyo ikajikita kwenye migogoro ya wakulima na wafugaji na kuachana na matatizo mengine kwa sababu wanajiongezea kazi isiyo yao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.