Scorpion asomewa upya mashitaka

DPP alimwachia huru, polisi wakamkamata

Uhuru - - Mbele - NA MWANDISHI WETU

MTUHUMIWA Salum Njwete ëScorpioní, anayedaiwa kumtoboa macho Saidi Mrisho, amesomewa upya shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, muda mfupi baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kumfutia kesi ya awali.

Hayo yalijiri jana, katika mahakama hiyo, wakati Scorpion, ambaye ni mwalimu na mcheza kareti, alipofikishwa kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo, akitokea gerezani kutokana na shauri hilo kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Alipofikishwa mahakamani hapo, mshitakiwa huyo alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Adelf Sachore, ambapo Wakili wa Serikali, Munde Kalombora, alidai shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, Munde alidai DPP amewasilisha hati ya kutokuwa na

nia ya kuendelea kumshitaki mshitakiwa huyo.

Kutokana na hilo, Hakimu Sachore alikubaliana na ombi hilo, hivyo alimuachia huru mshitakiwa huyo.

Baada ya kufutiwa mashitaka na kuachiwa, Scorpion alikamatwa tena na kupelekwa mahabusu, ambapo ilipotimu saa 6.18 mchana, alipandishwa tena kizimbani mbele ya Hakimu Flora Haule.

Wakili wa Serikali, Chesensi Gavyole, alimsomea mshitakiwa huyo shitaka la unyangíanyi wa kutumia silaha, analodaiwa kulitenda Septemba 6, mwaka huu, maeneo ya Buguruni Shell, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Chesensi alidai siku hiyo, mshitakiwa huyo aliiba mkufu wa fedha wenye gramu 38, ukiwa na thamani ya sh. 60,000, bangili ya mkononi, fedha taslimu sh. 331,000 na pochi, vyote vikiwa na thamani ya sh. 476,000, mali ya Said Mrisho.

Inadaiwa kabla ya kutenda kosa hilo, alimtishia Mrisho na kisha kumchoma kisu machoni, tumboni na mabegani.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, Scorpion alikana tuhuma hizo, ambapo wakili wa serikali alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 2, mwaka huu, kwa kutajwa na kusema, mshitakiwa ataendelea kubaki rumande kwa kuwa shitaka linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Jana, mahakamani hapo baada ya mshitakiwa huyo kuondolewa mashitaka, kila mtu aliyekuwepo alikuwa na shauku ya kutaka kujua kilichojiri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.