Faida za kubana matumizi hizi hapa

Kuelekea mwaka mmoja wa JPM

Uhuru - - Mbele - NA MWANDISHI WETU MISHAHARA MINONO YAPIGWA MARUFUKU

MIONGONI mwa mambo muhimu yaliyoahidiwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itakayoundwa ni kusimamia vyema ubanaji matumizi.

Hivyo baada ya Rais Dk. John Magufuli kuingia madarakani, serikali yake imeanza kutekeleza kwa vitendo ahadi hiyo kwa kufanya mambo makubwa na ya kukumbukwa.

AFUTA SHEREHE ZA UHURU

Moja ya eneo aliloanza nalo ni kufuta kwa muda baadhi ya sherehe na fedha zake kuelekeza katika mambo ya msingi, ikiwemo ya huduma za jamii. Itakumbukwa ilikuwa ni kawaida kwa sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara kupambwa kwa kila aina ya shamra shamra.

Hata hivyo, Desemba 9, mwaka jana, kupitia taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ilisema Rais Dk. Magufuli amefuta sherehe za Uhuru, badala yake siku hiyo itasherehekewa kwa kufanya usafi nchi nzima.

Uamuzi huo wa rais ulikuwa ni katika kuzuia matumizi ya fedha yasiyokuwa na lazima. Pia ilikuwa ni hatua moja wapo ya kuimarisha usafi ili kuondokana na ugonjwa wa kipindupindu uliokuwa ukilikabili taifa kwa kipindi hicho na fedha nyingi kutumika kuhudumia wagonjwa.

Rais Dk. Magufuli aliagiza fedha zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya sherehe hizo, zitumike kwenye upanuzi wa barabara ya Morocco.

AFUTA SHEREHE ZA BUNGE

Uamuzi huo wa rais aliuchukua baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, kisha kukagua mashine za MRI na CT-Scan na kubaini kwamba hazifanyi kazi kwa kipindi kirefu.

Dk. Magufuli aliagiza zaidi ya sh. milioni 200, zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya uzinduzi wa Bunge la 11, zipelekwe Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda vya wagonjwa.

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa Bunge la 11, iliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma, Rais Dk.Magufuli alisema ni jambo jema kwa wabunge kujinyima ili kuwasaidia wagonjwa walioko Muhimbili.

“Nilipoambiwa zimechangwa shilingi milioni 225, kwa ajili ya sherehe, nikasema fedha hizo zipelekwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zikasaidie kununua vitanda.

“Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumejinyima sisi wenyewe, lakini tutakuwa tumewanufaisha wenzetu, ambao wana matatizo makubwa yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo,” alisema Rais Magufuli.

ASITISHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI

Rais Dk. Magufuli alitangaza kusitisha maadhimisho ya siku ya Ukimwi kitaifa, ambayo yalikuwa yafunguliwe mkoani Singida, Desemba mosi, mwaka huu.

Badala yake rais aliagiza fedha zote zilizotengwa na serikali pamoja na wahisani mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho hayo, zielekezwe kununua dawa kwa waathirika wa Ukimwi na vitendanishi.

“Serikali imesitisha maadhimisho ya mwaka huu, Singida, badala yake fedha zilizopangwa kwa ajili ya maadhimisho ziende zikanunue dawa za virusi vya Ukimwi, dawa za kudhibiti maambukizi ya ukimwi na vitenganishi,” ilisema taarifa hiyo.

Hivyo kutokana na kutolewa kwa agizo hilo, baadhi ya maofisa wa serikali waliokuwepo mkoani Singida, walitakiwa kurejea kwenye vituo vyao vya kazi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk.Fatma Mrisho, maadhimisho hayo yalipaswa kutanguliwa na maonyesho ya wadau, yatakayojumuisha huduma mbalimbali zikiwemo za utoaji elimu na burudani.

Dk. Fatma alisema huduma nyingine zilizopangwa kutolewa katika maadhimisho hayo ya wiki moja ni upimaji wa hiari wa watu zaidi ya 3,500, wanaoishi na virusi vya Ukimwi na utoaji ushauri nasaha, upimaji wa shingo ya uzazi, sukari, uzito, damu na kupata elimu itakayotolewa kupitia vikundi vya sanaa na burudani.

SHAMRASHAMRA ZA MUUNGANO ZASITISHWA

Ubanaji matumizi ya fedha za umma pia ulihamia kwenye sherehe za maadhimisho ya Muungano, ambapo Rais Dk. Magufuli aliahirisha sherehe hizo.

Uamuzi huo uliweza kuokoa zaidi ya Sh. bilioni mbili, kisha aliagiza zikatumike kwenye upanuzi wa barabara inayokwenda Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, Rais alisema siku hiyo itakuwa ya mapumziko kama kawaida, na Watanzania waiadhimishe wakiwa majumbani kwao au katika shughuli zao binafsi.

“Kufuatia kuahirishwa kwa shamrashamra hizo, Rais Magufuli ameelekeza kuwa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya kugharamia vinywaji, vyakula, gwaride, halaiki, burudani mbalimbali na hafla ya usiku, ambazo ni zaidi ya sh. bilioni mbili, zitumike kuanzisha upanuzi wa barabara ya ‘Mwanza – Airport’ katika eneo linaloanzia Ghana Quaters hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza,” ilieleza taarifa ya Ikulu kutoka Chato.

“Barabara hiyo inafanyiwa upanuzi ili kukabiliana na kero ya msongamano mkubwa wa magari, ambao unaathiri shughuli za kila siku za wananchi,” ilifafanua taarifa hiyo ya Ikulu.

Panga la kudhibiti matumizi makubwa ya serikali likahamia kwa vigogo waliokuwa wakilipwa mishahara minono.

Rais alitangaza kupangua upya mishahara mikubwa ya wafanyakazi wanaopokea hadi sh. milioni 40, akisema kuwa lengo ni kuhakikisha katika kipindi chake kusikuwepo watu wanaolipwa zaidi ya sh. milioni 15 kwa mwezi. Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo wakati akiongea na wananchi kwenye mkutano wa hadhara wilayani Chato, mkoani Geita, mwaka huu, alipokwenda mapumzikoni.

Rais Dk. Magufuli alitolea mfano wa mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17, kisha kuagiza mfanyakazi huyo afikishwe mahakamani.

Alisema serikali imejiandaa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9, kuanzia bajeti ijayo.

Hivyo alitangaza kuwa watumishi wanaolipwa mishahara mikubwa inayofikia sh. milioni 40, itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha mshahara usiozidi sh. milioni 15.

VITA DHIDI YA WATUMISHI HEWA

Wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa, Rais Dk. Magufuli aliwapa siku 15, kuwaondoa watumishi hewa waliopo kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma katika mikoa yao.

Aliwataka washirikiane na Wakurugenzi wa Halmashauri kuwaondoa watumishi hewa.

“Nimewapa siku 15, kuanzia leo, mkashirikiane na Wakurugenzi wa Halmashauri zenu kuwatoa wafanyakazi hewa, nikigundua kuwa bado kuna wafanyakazi hewa, Mkurugenzi husika atafukuzwa kazi na atapelekwa mahakamani.

“Nimeamua kuwachagua nikiamini kwamba, mtaniwakilisha vizuri katika mikoa yenu, nawaomba mkatimize majukumu yenu bila kuogopa,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli alisikitishwa na taarifa ya uchunguzi kuhusu watumishi hewa, katika mikoa ya Singida na Dodoma, ambapo iligundulika watumishi 202, wanalipwa mishahara hewa.

Wakati wa utafiti huo, zaidi ya watumishi 26,900, walioko katika Halmashauri 14 za mikoa hiyo, watumishi 3,320, hawakuwepo kazini kwa sababu mbalimbali.

Kwa mantiki hiyo, ukichukua utafiti huo wa mikoa miwili ni dhahiri serikali inapoteza fedha nyingi kwa kulipa mishahara ya watumishi hewa nchi nzima.

Hivyo Dk. Magufuli aliwasisitiza wakuu wa mikoa wakasimamie ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa waliahidi kutatua kero za wananchi na wahakikishe wanazitatua ili wananchi waishi vizuri kwa amani ndani ya nchi yao.

Itaendelea…

“Nilipoambiwa zimechangwa shilingi milioni 225, kwa ajili ya sherehe, nikasema fedha hizo zipelekwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zikasaidie kununua vitanda. “Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumejinyima sisi wenyewe, lakini tutakuwa tumewanufaisha wenzetu, ambao wana matatizo makubwa yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo,”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.