Barabara ya Pofo/ Kilema kujengwa kwa changarawe

Uhuru - - Habari - NA WILIUM PAUL, MOSHI

HALMASHAURI ya Mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro, ipo katika harakati za mwisho za ujenzi wa barabara yenye ukubwa wa kilomita 12, kwa kiwango cha changarawe, kutoka kijiji cha Pofo, Mandaka hadi Kilema.

Imeelezwa kuwa, ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kuondoa adha kwa wananchi kutokana na ubovu uliopo sasa kwenye barabara hiyo.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 485.46, na unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi, Butamo Ndalahwa, alisema lengo la mradi huo ni kuboresha miundombinu ili kurahisisha utoaji wa huduma za kijamii, kiuchumi na kiusalama na kuondoa kero zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Mkurugenzi huyo alimtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi wa barabara hiyo, kuijenga kwa kiwango cha juu kulingana na mkataba walioandikishana na halmashauri.

“Muda uliobaki ni mdogo ikilinganishwa na kazi yenyewe, kwani unapaswa kuikabidhi barabara hii mwezi Novemba. Sasa nikuombe jaribu kuongeza nguvu na kasi, angalau katapila zifikie mbili ili uwe na kasi ya kumaliza kazi hii kwa haraka zaidi, kutokana na muda wa mkataba kuelekea kumalizika,”alisema Ndalahwa.

Kwa upande wake, mkandarasi anayesimamia ujenzi wa barabara hiyo kutoka Kampuni ya Termite Investment Ltd, Mhandisi Loomon Olesingo, alisema changamoto kubwa wanayoipata ni kukosekana kwa maji ya uhakika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.