Serikali: Hatuangalii sura kwenye uteuzi

n Vigogo 207 waomba ukurugenzi mkuu wa Shirika la Posta

Uhuru - - Mbele - NA WILLIAM SHECHAMBO

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema serikali ya awamu ya tano haiangalii sura ya mtu linapokuja suala la uteuzi wa nafasi nyeti kwenye taasisi muhimu serikalini.

Amesema kuna umakini wa hali juu, ndio sababu taasisi 29, zilizo chini ya wizara yake, 26 zilizopewa wasimamizi ni watu makini, ambao utendaji wao wa kazi tangu kuteuliwa kwao unapongezwa na wadau.

Profesa Mbarawa, alitoa kauli hiyo jana, mjini Dodoma, dakika chache baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kumteua Mhandisi James Kilaba, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Profesa Mbarawa alisema wajumbe wa kamati hiyo hawajakosea kutoa pongezi hizo kwa sababu kazi yake inaonekana pamoja na wenzake walioteuliwa kwenye nafasi kama hiyo katika taasisi zingine, zikiwemo Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).

Alisema lengo la serikali ni kuwa na wasimamizi na watendaji kwenye taasisi zake, ambapo mpaka sasa Wizara ya Ujenzi imebakiza taasisi tatu kati ya 29, kuteua wakurugenzi wakuu, ambapo mpaka Januari, mwakani, zitakuwa zimekamilika.

“Kati ya taasisi 29, zilizo chini ya wizara yangu, tatu bado ndizo zinasubiri serikali iteue wakurugenzi wake wakuu na hizi ni Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL),” alisema.

Waziri huyo alisema serikali ya Rais Dk. John Magufuli, haina urafiki kwenye kuteua wasimamizi wa taasisi ndio sababu mpaka kufikia jana, waombaji nafasi moja ya ukurugenzi mkuu wa Shirika la Posta wamefikia 207.

Awali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakati ikitoa pongezi kwa serikali kwa uteuzi makini wa wasimamizi wakuu wa taasisi nyeti zinazogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania, ilisema matumaini yapo.

Ilisema taasisi hizo zilizopewa watu makini ni pamoja na zile zilizoko chini ya usimamizi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inayoongozwa na Waziri Mbarawa.

Akitoa pongezi hizo muda mfupi baada ya kamati hiyo kusikiliza majibu ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Kilaba, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso, alisema kamati imeridhishwa na utendaji kazi wa TCRA.

Alisema mkurugenzi huyo amejibu hoja za wana kamati, hususan masuala ya wizi wa mtandao, kitaalamu na kwamba anajua anachokifanya.

Alisema kamati yake inapata faraja kwa kupewa mtu makini kusimamia taasisi hiyo (TCRA), ambayo inagusa maisha ya kila mtanzania kwa wakati huu, ambao huduma za mawasiliano zinashika kasi.

“Tunashukuru kwa majibu mazuri ya Mkuu wa TCRA, ambaye bila shaka ni mtu makini. Waziri (Mbarawa) hongera tunawaomba mwendelee kuwa pamoja na kamati hii,” alisema.

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, jana, iliitwa mbele ya Kamati ya Miundombinu, kutoa taarifa yake kuhusu masuala mbalimbali, yakiwemo yanayohusiana na uhalifu wa mtandaoni, ambapo Mhandisi Kilaba alisema jitihada zinafanyika kwa ushirikiano na wadau wengine wa usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi.

“Wizi wa mtandaoni ni kama wizi mwingine, isipokuwa huu unatumia njia za kielektroniki, hivyo tunashirikiana na polisi, kampuni za simu kuhakikisha kila miamala ya kihalifu inanaswa,” alisema.

Alitoa mfano, alisema mwaka jana, aliyekuwa Naibu Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba, alitoa takwimu za fedha zilizoibwa kwa wizi wa mtandao, lakini takwimu hizo zilitoka polisi na sio TCRA, hivyo ushirikiano ni lazima.

WANAFUNZI wa ugani katika Chuo cha Kilimo na Mifugo, kinachomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya (CCM), Kaole, Bagamoyo, mkoani Pwani, wakimwagilia mashamba ya mfano chuoni hapo, juzi. (Picha na Christopher Lissa).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.