Wanafunzi 45,000 wadahiliwa TCU

Uhuru - - Mbele - NA RACHEL KYALA

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imefungua udahili awamu ya nne katika fani mbalimbali, utakaojumuisha wanafunzi 45,000, kutokana na wanafunzi wengi kutopata udahili katika vyuo mbalimbali nchini.

Wanafunzi wametakiwa kuondoa dhana potofu juu ya fani wanazopaswa kusoma, kulingana na michepuo ya masomo waliyochukua sekondari, kutokana na kuwepo ufinyu wa uelewa juu ya wigo wa fani kwa masomo fulani.

Kaimu Mkurugenzi- Udahili, Dk. Kokuberua Mollel, akizungumza jijini Dar es Salaam, jana, alisema hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa wanafunzi wenye sifa, ambao hawajapata udahili kutokana na ushindani uliopo katika fani walizoomba awali.

ìUdahili huu utadumu kwa siku tatu tu na utafunguliwa kuanzia Jumatatu, wiki ijayo. Majina ya watakaochaguliwa yatapelekwa katika vyuo husika na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB) kwa ajili ya kupatiwa mikopo,î alisema.

Alisema wanafunzi ni lazima wapanuke uelewa juu ya fani wanaoweza kuchukua na siyo kukariri, ambapo alitoa mfano kuwa wanafunzi karibu wote waliosoma mchepuo wa masomo ya Fizikia, Kemia na Baolojia (PCB), wanataka kusomea udaktari.

“Hii ni dhana potofu, suala hilo limesababisha ushindani mkubwa kwani nafasi za kusomea udaktari zilizopo nchini ni 2,500 tu, lakini walioomba ni zaidi ya 10,000, hivyo

waliodahiliwa ni wale waliopata alama za juu zaidi ingawa wote walioomba wanazo sifa,” alisema.

Dk. Kokuberua aliwataka kutambua kuwa, zipo fani nyingine nyingi wanazoweza kusomea mbali na udaktari na kwamba, waliosoma lugha wanapaswa kusomea fani nyingine, badala ya sheria kama inavyodhaniwa na wengi.

Hata hivyo, alisema serikali inafanya jitihada za kuongeza nafasi katika fani ya udaktari kulingana na uhitaji, ambapo tayari kimeanzishwa Chuo cha Mloganzila na vyuo vilivyofungiwa kufunguliwa iwapo vitakidhi vigezo.

Alieleza kuwa awamu ya kwanza ya udahili, walidahiliwa wanafunzi 30,733 na kubaki 26,000, awamu ya pili walidahiliwa 27,900 na kubaki 6,420, awamu ya tatu ni 1,119 na kusalia wanafunzi 4,500.

Mkurugenzi huyo aliwataka wanafunzi kuwa makini kuangalia ni fani zipi wanazoweza kuomba, ambazo bado zina nafasi ili kuepuka kukosa fursa hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.