Wasomi wazidi ‘kumfagilia’ kwa kutoa elimu bure

Uhuru - - Mbele - NA SIMON NYALOBI

RAIS Dk. John Magufuli, amepongezwa kwa kufanikisha mpango wa utoaji wa elimu bure na madawati shuleni, kwa kipindi cha mwaka mmoja alichokaa madarakani. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Silivester Rugeihyamu, alitoa pongezi hizo Dar es Salaam jana, wakati akitoa tathmini ya elimu kwa mwaka mmoja wa Rais Magufuli, tangu aingie madarakani.

Dk. Rugeihyamu alisema, Rais Magufuli anastahili pongezi hizo, kwani ameonyesha umahiri katika kusimamia nyanja hizo.

“Kwa haya mambo, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa, serikali imebeba mzigo wa elimu na madawati kwa wazazi,

“Amerudisha mfumo wetu wa zamani tuliosoma bila ya kulipia, lakini tofauti tu sisi tulipewa kalamu na vitabu bure,” alisema.

Alisema kuwa, kwa sasa wazazi wamesahau mzigo wa kulipia ada, pamoja na michango, ambayo iliwatesa katika kuwasomesha watoto wao.

Akizungumzia vitu vya kuongezwa, katika mfumo wa elimu bure, alishauri serikali kuongeza utoaji wa vitabu na kalamu bure kwa wanafunzi.

Alifafanua kuwa, sasa mzigo kwa wanafunzi uko katika vitendea kazi hivyo, ambavyo vinauzwa kwa bei kubwa.

Mhadhiri huyo alisema, licha ya mafanikio yaliyopatikana katika madawati, serikali ni budi ikahamishia nguvu zake katika ujenzi wa madarasa.

“Sasa hivi madawati yamekuwa mengi na tumeona baadhi ya shule zimeshindwa kuyaweka katika madarasa, kutokana na uhaba wa madarasa, sasa ni bora juhudi zielekezwe kujenga madarasa,” alisisitiza.

Kuhusu fungu la fedha linalopelekwa shuleni kwa ajili ya mahitaji ya shule, alisema kuna haja ya kufanyika kwa tathmini juu ya fedha hizo iwapo zinatosheleza au la.

Kwa mujibu wa Dk. Rugeihyamu, mahitaji ya shule ni mengi, ikiwemo ya gharama za ulinzi wa shule na vitendea kazi, hivyo zinaweza kuwa kubwa kuliko matarajio ya serikali.

Aidha, alisema fedha zinavyotumika zinapaswa kufanyiwa tathmini iwapo zimeleta maendeleo yaliyokusudiwa katika shule husika.

Pia, alishauri serikali kutazama upya kibali cha michango ya dharura na uboreshaji elimu, ili ipewe kamati ya shule, badala kutolewa na Mkuu wa Mkoa.

Vilevile, kuhusu wanafunzi kuhimizwa kusoma masomo ya sayansi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, anashauri serikali kuweka mpango wa kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya sayansi.

RAIS Dk. John Magufuli

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.