Kamati ya bunge yaitunishia misuli serikali

Uhuru - - Mbele -

KAMATI ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira, imetishia kutoshirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, kama ofisi hiyo haitakuwa tayari kufanya ziara kwenye maeneo ya migodi na mabonde.

Pia, imegoma kujadili taarifa ya utupaji taka katika migodi iliyokuwa iwasilishwe na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, kwa madai kuwa inaonekana kuwa na upungufu mkubwa na kuwemo kwa taarifa za uongo.

Mbali na hilo, kamati hiyo imesema sababu nyingine iliyosababisha kukataa kuijadili taarifa hiyo ni pamoja na wabunge kutoshirikishwa katika ziara kwenye maeneo ya migodi ili kujionea hali halisi ya utupaji taka.

Mbunge wa Viti Maalumu,Tauhida Galoss Nyimbo (CCM), alisema wabunge hawapo tayari kufanya kazi za serikali ili kuwafurahisha mawaziri na timu zao, bali wapo kwa ajili ya kusimamia serikali kwa maslahi ya wananchi.

Alisema kamwe kamati hiyo haiwezi kujadili taarifa, ambayo ilitakiwa kuwasilishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa kuwa kamati hiyo zaidi ya mwaka mmoja sasa, haijafanya ziara kwenye maeneo ya migodi na sehemu za mabonde.

“Hivi hapa Naibu Waziri na timu yako mnatuletea hii taarifa tujadili kitu gani au nyie wizara hamjui wajibu wenu. Hivi kweli mnadhani sisi ni wasaidizi wenu au tunafanya kazi za serikali.

“Sisi hatufanyi kazi za serikali, bali tunafanya kazi ya kuisimamia serikali na kutetea maslahi ya Watanzania waliotutuma tuwawakilishe na kuwatetea hapa bungeni.

“Mmetuletea hii taarifa imejaa mipicha mitupu, sasa sisi tunawezaje kujadili kwa kukubali au kukataa, kwa maana sisi hatujafika hata katika kiwanda kimoja kujua hizo taka za sumu zinasambazwaje na kutunzwa wala hatujui zinawaathi vipi wananchi wa maeneo hayo,”alihoji.

Mbunge wa Moshi Mjini, Anthony Komu (CHADEMA), aliunga mkono kukataliwa kwa taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa madai kuwa, iwapo watajadili taarifa hiyo, watakuwa hawawatendei haki wananchi.

Alisema taarifa ya taka sumu katika migodi ni sawa na kusoma kitabu cha hadithi au kusoma gazeti, kwani ukiwa unasoma vitabu hivyo kamwe huwezi kuhoji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima (CCM), alisema ripoti hiyo haionyeshi malengo, ambayo yameshafanywa na serikali na pia hawana uelewa mpana kuhusu mazingira ya nchi, hivyo wanahitaji kufika kwenye maeneo husika ndipo warudi kuijadili ripoti hiyo.

Alisema wizara inawaletea ripoti zenye mapicha wakati wao wanataka uhalisia ndio maana wajumbe wa kamati hawako tayari kujadili kitu ambacho hawakijui na hawajawahi kukiona.

Makamu Mwenyekiti wa kamati, Vicky Kamata, akizungumza katika kikao hicho, alisema hawawezi kupitisha ripoti hiyo kwani watakuwa wanajidanganya wao na wananchi, ambao wapo kwa ajili ya kuwawakilisha.

Vicky alisema endapo serikali haina pesa za kuwapeleka kufanya ziara, ifute kabisa kamati zisiwepo kwani itakuwa haina maana kujadili kitu, ambacho hawajawahi kukiona kwa uhalisia.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, alisema wizara yake imeonewa kwani siyo jukumu lake kuratibu ziara za kamati na wala siyo jukumu la ofisi ya makamu wa rais, isipokuwa ni jukumu lao wenyewe kamati kusema kama wanataka kufanya ziara.

Alieleza kushangazwa na wabunge wenzake kwa kutoomba ziara ya kwenda kutembelea migodi, maeneo yaliyoathirika na mabonde ili wayaone mazingira yalivyo na jinsi sumu zinavyoathiri mazingira.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.