Tishio la uhaba wa chakula, magonjwa ya milipuko laja

Uhuru - - Mbele - JESSICA KILEO NA EZEKIEL DIMOSO (RCT)

SERIKALI imetoa wito kwa wadau kuchukua tahadhari ili kukabiliana na athari zitakazotokana na kuchelewa kwa mvua kwenye maeneo mengi nchini.

Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa.

Ilisema wizara, taasisi za serikali, mamlaka za mikoa na wadau wengine wa usimamizi wa maafa, wanapaswa kuchukua hatua muhimu ili kukabiliana na athari zitakazotokana na kuchelewa kwa mvua kwenye maeneo mengi nchini.

Pia, zimetakiwa kuhakikisha ulinzi na usimamizi wa kina unakuwepo ili kusitokee ufichwaji wa vyakula na upandishwaji wa bei ya vyakula kiholela kwa kipindi, ambacho kutatokea athari zitokanazo na ukame.

Hayo yalisemwa jana, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu utabiri wa hali ya hewa uliotolewa Septemba 5, mwaka huu.

Brigedia Msuya alisema utabiri huo ulibainisha kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba, mwaka huu, kwamba kutakuwa na uhaba wa mvua kwenye maeneo mengi nchini.

Msuya alisema kwa mujibu wa utabiri huo, katika miezi mitatu hiyo, kutakuwa na upungufu wa mvua, hivyo kunaweza kutokea athari nyingi ikiwemo ukame.

ìIli kukabaliana na athari zitakazojitokeza, wizara, taasisi za serikali, mamlaka za mikoa na wadau wengine wa usimamizi wa maafa wanatakiwa kuhimiza na kulima mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame,” alisema.

Pia, aliagiza kuhusu umuhimu wa kuhifadhi chakula vizuri, kuzuia matumizi ya nafaka kutengeneza pombe na kuwahimiza wananchi kuweka akiba ya chakula cha kutosha, hasa kwa maeneo yatakayopata mvua chini ya wastani.

Mkurugenzi huyo alisema pia kuwa, wanatakiwa kuchimba au kukamilisha na kukarabati mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua.

Alizitaka mamlaka za hospitali na zahanati, kujiandaa kukabiliana na magonjwa ya milipuko endapo yatatokea.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk. Paschal Waniha, alisema mvua chache zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, wakati maeneo ya pembozoni mwa Ziwa Victoria na yale ya kusini mwa nchi yakiwa na mvua nyingi.

Alisema mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika ukanda wa Ziwa Victoria na katika maeneo machache ya pwani ya kaskazini, katika mwezi Oktoba, mwaka huu.

ìKatika maeneo mengi nchini, mvua zinatarajiwa kuchelewa kuanza, hii imetokana na tathmini ya mifumo ya hali ya hewa inayoonyesha uwepo wa La-Nina hafifu katika eneo la Bahari ya Pacific.

“Kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, msimu wa mvua umeanza katika maeneo machache ya ukanda wa Ziwa Victoria japo bado ziko chini,îalisema.

Alibainisha athari zitakazoweza kujitokeza kuwa ni vipindi virefu vikavu, vina vya mito na mabwawa vitapungua, milipuko ya magonjwa na uhaba wa malisho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mary Stela Mtalo, alisema kutokana na utabiri huo, kitengo hicho kitakuwa kinafuatilia na kukusanya taarifa ya chakula nchini kila wakati.

Alisema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NRFA), unatakiwa kununua na kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha ili kukabiliana na upungufu huo kutoka kwenye maeneo yenye ziada mapema.

Mary Stela alisema Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko

inatakiwa kununua mazao ya wakulima kwa wingi ili kuongeza wigo wa biashara na soko la mazao ya wakulima sambamba na kuyaongezea thamani.

Pia, alisema mikoa na halmashauri zake zinapaswa kusimamia na kuimarisha mifumo ya kuhifadhi chakula baada ya mavuno ili kupunguza upotevu wa chakula na kuhakikisha upatikanaji wake wakati wote.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.