Mfalme wa Morroco kuja nchini Jumapili

Uhuru - - Habari - NA RACHEL KYALA

MFALME wa Morroco, Muhammed wa 6, anatarajiwa kufanya ziara ya siku tatu nchini, kuanzia Jumapili ijayo, ambapo nchi hiyo itatiliana saini na Tanzania, mikataba 16 ya kiuchumi.

Aidha, mfalme huyo anatarajiwa kuja na ujumbe wa zaidi ya watu 150, wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wa nchi hiyo, maofisa wa serikali na sehemu ya familia yake, ambapo baada ya ziara ya kikazi, watafanya utalii katika vivutio mbalimbali nchini, ikiwemo visiwani Zanzibar.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga, akizungumza jijini Dares Salaam, jana, alisema baada ya ziara ya kikazi, mfalme huyo atapumzika na kufanya utalii katika mbuga za wanyama na sehemu nyingine kwa siku tano, kabla ya kuondoka.

“Mikataba itakayotiwa saini itahusu serikali na sekta binafsi, ikiwemo taasisi za dini na vyuo. Nchi hii ni ya tano kwa uchumi mkubwa barani Afrika mbali na Afrika Kusini, Nigeria, Angola na Misri, ambapo yenyewe inakaribiana na Algeria,” alisema.

Alisema Tanzania imekuwa ikijenga uhusiano wa diplomasia ya uchumi na nchi inazoona zipo juu kiuchumi kama fursa ya kunufaika kimaendeleo.

Mahiga alisema Morroco ipo vizuri katika sekta za utalii, miundombinu, hususan ya nishati, ulinzi, madini na elimu katika ustawi wa jamii, ikiwemo benki na katika sekta ya fedha.

“Awali, Tanzania ilikuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Morroco kupitia ubalozi wetu nchini Ufaransa na wao kupitia ubalozi wao nchini Kenya, lakini sasa tumeona ni vyema nchi hizi mbili zikawa na uhusiano wa moja kwa moja na kuukuza katika nyanja za uchumi na biashara,” alisema Mahiga.

Alisema kutakuwepo mkutano baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Morroco siku moja kabla ya kuwasili nchini kwa mfalme huyo, ambapo tayari ujumbe wa takribani wafanyabiashara 100, umeshawasili.

“Baada ya kuwasili, Mfalme Muhhamed wa 6, atakuwa na mazungumzo, Ikulu, Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Dk. John Magufuli, ikiwemo kuandaliwa hafla ya chakula cha jioni, pia atakwenda Zanzibar ambapo atakuwa na mazungumzo na Rais Dk. Ali Mohammed Shein,” alisema.

Aidha, Waziri Mahiga alisema Morroco ilionyesha nia ya kurudi katika Umoja wa Afrika (AU), baada ya kujitoa kwa kipindi cha miaka 36, kwenye umoja huo, ambapo awali ulijulikana kama OAU.

“Tulipokea waraka wa Mfalme huyo wa kutaka Rais wetu amuunge mkono ili Morroco ikubaliwe kurudi AU. Katika mkutano wa umoja huo unaotarajiwa kufanyika Januari, Addis Ababa, Ethiopia, miongoni mwa sababu ni kuwa nchi hiyo inao ushirikiano mzuri wa kiuchumi na nchi nyingi za Afrika,” alisema waziri huyo.

Alitaja mambo mengine yatakayofanyika wakati wa ziara ya kiongozi huyo wa Morroco, ambaye pia ni msimamizi wa madhehebu ya dini nchini kwake, kuwa ni kuweka jiwe la msingi la Msikiti wa BAKWATA, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alisema ni mara ya kwanza kwa Tanzania kutembelewa na mfalme, hivyo ni ujio rasmi na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki mfalme huyo anayetokea Rwanda ambapo baada ya ziara yake Tanzania, anatarajiwa kwenda Kenya na Ethiopia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.