TABOA yailalamikia SUMATRA

Uhuru - - Habari -

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kimeyalalamikia mapendekezo yaliyowasilishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), kwa ajili ya marekebisho ya Sheria ya Leseni za Usafirishaji na kudai yarekebishwe au kuondolewa.

Malalamiko hayo yalitolewa mjini hapa jana, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu, wakati akitoa maoni ya chama hicho kuhusu mapendekezo ya kurekebisha sheria hiyo.

Alisema endapo mapendekezo ya kuirekebisha sheria ya leseni za usafirishaji yataachwa na kupitishwa, Watanzania watakabiliwa na tatizo kubwa la usafiri.

Mrutu alisema mapendekezo ya mamlaka hiyo hayana lengo la kuboresha sheria hiyo, bali yamelenga kuwakomoa wamiliki hao na kuongeza zaidi tatizo la usafirishaji nchini.

Chama hicho kilitumia nafasi hiyo kuiomba serikali ya awamu ya tano, isiipatie SUMATRA, mamlaka ya kukusanya mapato kwa wadau wa usafirishaji, badala yake masuala yote ya fedha ya usafirishaji yasimamiwe na mamlaka husika kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Pamoja na kwamba mamlaka hiyo haikuwashirikisha wadau wa usafirishaji tangu mwanzo wa mchakato wa marekebisho ya sheria hiyo, baada ya kuyapitia mapendekezo yaliyowasilishwa na SUMATRA,TABOA inayapinga na kuyakataa,”alisema.

Akizungumzia baadhi ya mapendekezo yatakayofanyiwa marekebisho kwenye sheria hiyo, aliyataja kuwa ni pamoja na kupandishwa kwa tozo kubwa ya faini kutoka kiwango cha chini cha sh.10,000 hadi sh. 200,000, na kiwango cha juu sh.20,000 hadi sh.500,000, kwa msafirishaji atakayekiuka masharti ya leseni za usafirishaji.

Katibu huyo alibainisha kuwa, pendekezo hilo limelenga kuwakomoa wasafirishaji kwani wengi wao pamoja na kutaabika na gharama za uedeshaji mabasi yao, pia wana mlolongo wa tozo wanazolipa, ikiwemo kodi za bima, leseni, ratiba za usafiri na kulipia logo.

Alisema pamoja na tozo hizo, tofauti na wasafirishaji wa malori, wasafirishaji wa abiria hulazimika kulipa tozo kwa kila halmashauri ambako basi linapita.

Alieleza kuwa mapendekezo hayo katika kipengele cha faini, yametaka mmiliki ataifishwe gari endapo atafanya makosa mbalimbali, ikiwemo ajali za barabarani na kukiuka masharti ya leseni yake, hali ambayo itazidi kuwadidimiza.

Katibu huyo alitaja mapendekezo mengine wanayoyapinga na kutaka yafanyiwe marekebisho kuwa ni pamoja na kutoa adhabu kwa kosa linalofanywa na basi moja kwa kampuni nzima, hali inayozorotesha uchumi wa kampuni husika.

Wajumbe wa kamati hiyo waliunga mkono hoja za chama hicho na kuahidi kuzishughulikia ili marekebisho ya sheria hiyo yafanyike kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bukene, Seleman Zed (CCM), alisema kamati hiyo haitatoa hukumu kuhusu suala hilo, bali itachukua mapendekezo ya pande zote mbili na baadaye kuyajadili na kuyawasilisha serikalini kwa ajili ya utekelezaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.