Mdahalo watawaliwa na vioja lukuki

Uhuru - - Habari - NEW YORK, Marekani

MDAHALO wa kihistoria kwa wagombea urais wa Marekani, kupitia Republican, Donald Trump na mwenzake wa Democratic, Hillary Clinton umetawaliwa na vioja lukuki na kuzuliana kashfa.

Kioja kikubwa kilichowashangaza wengi ni pale Trump alipokataa kuahidi kukubali matokeo ya uchaguzi iwapo atashindwa.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mbinu ya Trump kutaka kuaminisha umma kuwa aliibiwa kura kama ambavyo amekuwa akisisitiza kabla Wamerekani hawajaamua ni nani atayakeliongoza taifa hilo.

Mjadala huo uliorushwa moja kwa moja kupitia luninga, uliofanyika kwenye jimbo la Las Vegas, Trump alimuita Hillary kuwa ni mwanamke muovu.

Kauli hiyo iliyolenga kumchafua mpinzani wake ameitoa kufuatia matokeo ya kura za maoni kuonyesha umaarufu wa Trump umezidi kuporomoka baada ya kukabiliwa na tuhuma za unyanyasaji wa kingono.

Wagombea hao walikataa kusalimiana kwa mikono kabla na baada ya majibizano hayo ya kisiasa, hatua iliyogeuza mjadala huo kutawalia na kelele za mabishano za wagombea hao.

Trump alitoa ahadi kwa wanachama wa Republican kuwateua majaji wa mahakama ya juu zaidi wanaoegemea mrengo wa kihafidhina watakaobadili sheria inayohalalisha utoaji mimba na kulinda haki za kumiliki silaha.

Alisisitiza ahadi yake ya kuwarudisha nyumbani wahamiaji ambao hawakusajiliwa na kudhibiti mipaka ya Marekani.

Naye Hillary alitangaza wazi kuwa, atawatetea wapenzi wa jinsia moja, atalinda haki za utoaji mimba, atawainua watu wa kipato cha wastani na kushinikiza kulipwa sawa kwa wanawake.

Alisema serikali haina shughuli yoyote katika maamuzi wanayofanya wanawake, hivyo haitaingilia masuala ya msingi yanayowalenga.

Katika mojawapo ya nyakati zilizokuwa na mvuto, Trump alikataa mara mbili kusema iwapo atakubali matokeo ya uchaguzi, hatua iliyobadili utamaduni wa muda mrefu wa wagombea wanaoshindwa kukubali matokeo baada ya kura kuhesabiwa.

Baada ya Trump kushindwa kufanya hivyo, Hillary alitoa angalizo kuwa, kitendo hicho alichofanya mgombea mwenzake ni cha kuogopwa.

“Anaponda na kudharau demokrasia yetu. Na mimi kivyangu, nimeshangazwa kuwa mtu ambaye ni mgombea mteule wa mojawapo wa vyama viwili vikuu, anaweza kuchukua msimamo wa aina hiyo,” alisisitiza Hillary.

Majibu ya Trump yamezusha shutuma kali kutoka kwa Seneta wa Republican, Lindsey Graham, aliyesema mgombea huyo hawajibiki ipasavyo kwa chama chake na taifa kwa kuendelea kuamini anafanyiwa udanganyifu katika uchaguzi ujao.

Alisema Trump analazimika kutafuta namna ya kujitenga dhidi ya tuhuma za unyanyasaji wa kingono.

Kwenye mdahalo huo, Trump alisisitiza kuwa wanawake wanaomshutumu kuwanyanyasa kingono, ni watu wanaotaka kujulikana au wafuasi wa kampeni za Hillary huku akimuita mgombea huyo mwanamke muovu.

Pia Hillary alilazimika kujitetea kuhusu barua pepe zake, wakfu wa familia yake na taarifa za aibu zilizofichuliwa katika mtandao wa Wikileaks.

Kuhusu swali lililoulizwa iwapo Trump atakana kuitambua serikali ya Russia ambayo maofisa wa Marekani wanasema ndiyo inayohusika na uvamizi wa mitandao, Trump alisema hajaonana na Putin (licha ya kujigamba katika mjadala wa chama chake kuwa alizungumza naye katika chumba kimoja cha televisheni).

Alisema Hillary ni muongo na ndiye ‘kinyago’ cha kweli kinachoendeshwa na Russia.

Swali kuhusu ulipaji kodi wa kila mgombea, na majibizano kuhusu nani anayepunguza au kuongeza kodi zaidi ya mwenziwe, Trump alimkabili Hillary kuhusu makubaliano yake ya kibiashara ya siku za nyuma.

Alihoji kwa nini Clinton hakuidhinisha mageuzi anayopendekeza sasa miaka 30 ya nyuma alipokuwa akiitumikia serikali.

“Ulihusika na kila suala la nchi hii. Na una uzoefu, hilo ndio jambo unalonizidi lakini ni uzoefu mbaya kwa sababu ulichokifanya mpaka sasa kimegeuka kuwa kibaya.” Trump alieleza.

Lakini naye Hillary alimgeukiwa Trump akieleza kuwa, wakati akitetea haki za watoto miaka ya 1970, Trump alikuwa anajitetea katika kuwanyanyasa raia weusi wa Marekani katika mradi wa nyumba.

Aliongeza pindi alipokuwa akitetea haki za wanawake miaka ya 1990, Trump alikuwa anamkejeli mshindi wa maonyesho ya urembo kuhusu uzito wa mwili wake.

Hillary alibainisha wakati alipokuwa ikulu ya White House akitazama shambulio dhidi ya Osama bin Laden, Trump alikuwa anaendesha kipindi kwenye runinga.

Maneno hayo yalimfanya Trump kupoteza mwelekeo kwenye mdahalo huo.

Baada ya mdahalo huo, maofisa wa Republican walionekana wazi kuwa na wasi wasi, kuzungumzia kauli ya Trump.

Hata hivyo baadhi yao walisema kauli hiyo ilikuwa ya utani huku wengine wakidai kuwa Trump hataki kufikiria kushindwa kabla ya uchaguzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.