Mashahidi tisa kuitwa kesi ya ‘Malkia wa Tembo’

Uhuru - - Habari - NA FURAHA OMARY

UPANDE wa Jamhuri unatarajia kuita mashahidi takriban tisa wakati wa usikilizwaji wa kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili raia wa China, Yang Glan, maarufu ëMalkia wa Meno ya Temboí na wenzake wawili.

Shauri hilo lililoko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, limepangwa kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande huo Novemba 4, mwaka huu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, alipanga jana, tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo, baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akishirikiana na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.

Mbali na Yang, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Salvinus Matembo na Manase Philemon, ambao wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kujihusisha na nyara za serikali, ambazo ni meno ya tembo yenye thamani ya sh. bilioni 5.4 na kutoroka chini ya ulinzi halali wa askari.

Awali, Wakili Kadushi aliwasomea mashitaka washitakiwa hao, ambayo waliyakana na baadae aliwasomea maelezo ya awali, ambapo walikubali taarifa zao binafsi tu.

Akiwasomea maelezo hayo, ambayo yote waliyakana, Kadushi alidai kabla ya Aprili 20, 2014, maofisa wa Polisi Tanzania walipokea taarifa za Kiinterejensia kwamba, nchini kuna mtandao mkubwa wa uhalifu wa kukusanya meno ya tembo kutoka kwa majangili wadogo na hatimaye kuyasafirisha kwenda Bara la Asia.

Alidai mshitakiwa Manase alikamatwa Aprili 20, 2014 na polisi na muda mfupi alikiri kukusanya, kununua na kusafirisha meno ya tembo kwenda nchi za nje kwa kushirikiana na washitakiwa wenzake, Yang na Matembo.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba, mshitakiwa huyo alikiri zaidi kuwa akiwa na Matembo, walikuwa wakikusanya meno ya tembo kutoka kwa majangili wadogo na mnunuzi mkubwa alikuwa Yang.

Kadushi alidai uchunguzi zaidi uliendelea, ambapo Matembo na Yang walikamatwa na wao walikiri tuhuma hizo.

Alidai Manase na Matembo, kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014, kwa pamoja huku wakijua walijihusisha na mtandao huo, kazi yao ikiwa kukusanya meno hayo na mnunuzi wao alikuwa Yang na walifanya hivyo bila ya kuwa na kibali au leseni yoyote na lengo lao ni kupata faida.

Kadushi alidai uchunguzi huo ulibaini kwamba, Yang ushiriki wake ulikuwa ni kuratibu na kufadhili shughuli zote za mtandao wa uhalifu uliosababisha ukusanyaji, usafirishaji na uuzaji wa vipande 706, vya meno ya tembo kwenda nje ya nchi bila ya kuwa na kibali au leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Wakili huyo alidai upelelezi huo ulibaini meno hayo ya tembo yalivyokuwa yakisafirishwa, yakihifadhiwa na Yang na alivyokuwa akifanya malipo anaponunua meno hayo.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Dk. Masumbuko Lamwai, alipinga baadhi ya maelezo akidai kwamba, hayakustahili kuwepo katika hatua hiyo ya usikilizwaji wa awali.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri ulipingana na hoja hiyo na kudai kwamba, mshitakiwa ndiye anayepaswa kueleza kile anachokubali au anachokataa na si wakili kusema kwa niaba yake.

Baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote, Hakimu alisema kwamba kazi ya uuandaji wa maelezo hayo ya awali ni ya upande wa Jamhuri na kwamba, hakuna upande ambao unaweza kuwaelekeza cha kufanya.

Kutokana na maelezo hayo, Hakimu aliwahoji washitakiwa kile wanachokubali katika maelezo hayo, ambapo walikubali taarifa zao binafsi tu.

Wakili Kadushi alidai wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, wanatarajia kuita mashahidi takriban tisa.

Kwa upande wa mawakili wa utetezi, Dk. Lamwai, Jeremiah Ntobesya na Nehemiah Nkoko, walieleza kuwa watakuwa na mashahidi saba.

Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Novemba 4, mwaka huu kwa usikilizwaji na washitakiwa walirudishwa rumande.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kukutwa wakisafirisha vipande 706, vya meno ya tembo, vyenye uzito wa kilo 1,889, vikiwa na thamani ya sh. bilioni 5.4, bila ya kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Yang na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari mosi, 2000 na Mei 22, 2014. Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na uhalifu wa kupanga, kukusanya, kusafirisha na kuuza meno hayo ya tembo bila kibali.

Mshitakiwa Philemon anakabiliwa na shitaka la kutoroka akiwa chini ya ulinzi halali wa polisi, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 21, 2014, eneo la Sinza Palestina, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.