JPM aibukia semina ya madiwani Tabora

Uhuru - - Habari - NA ALLAN NTANA,TABORA

KAULI ya Rais Dk. John Magufuli ya kudai risti unaponunua au kuuza kitu chochote, imechukua sura mpya baada ya madiwani wa Manispaa ya Tabora, kuhoji sababu zinazokwamisha halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji mapato.

Akitoa mada juu ya ukusanyaji mapato, mratibu wa semina iliyohusisha madiwani na wakuu wote wa idara katika halmashauri hiyo, Hamis Mjanja, alisema bila kudai risiti, halmashauri hiyo haiwezi kupata mapato ya kutosha kwani mapato yao mengi yanaishia mifukoni mwa wajanja wachache.

Mjanja alisema suala la kuongeza mapato na ufanisi wa zoezi zima la ukusanyaji mapato, linategemea weledi wa watendaji wa halmashauri na umakini wa madiwani katika kusimamia shughuli hiyo, hivyo akawataka madiwani kuamka na kuisimamia halmashauri yao.

Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri, alisema wajibu wa madiwani na wakuu wa idara ni kutoa elimu na kuhimiza wananchi kudai na kutoa risiti wanapofanya biashara ili kuwezesha halmashauri hiyo kukusanya mapato kwa asilimia 100.

“Ninyi madiwani mnay o dhamana kubwa katika suala zima la ukusanyaji mapato na hili mnapaswa kulisimamia ipasavyo ili kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Dk. Magufuli,” aliongeza.

Hoja hiyo ilionekana kuwagusa madiwani hao huku baadhi wakiapa

kuchukua hatua na kuwa wakali kwa mkurugenzi wa manispaa hiyo na watendaji wake wote katika halmashauri hiyo, ikiwemo wahusika wote wa kukusanya ushuru katika vyanzo vya mapato ya halmashauri hiyo.

Akizungumzia namna madiwani wanavyoweza kuchochea ukusanyaji wa mapato, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi, alisema madiwani wanayo nafasi kubwa ya kufanikisha kazi hiyo kwa kuwa muda mwingi wapo karibu na wananchi.

Alisema kama madiwani watatambua wajibu wao na kusimamia shughuli zote za maendeleo katika kata zao, halmashauri itakusanya mapato kwa asilimia kubwa pasipo shaka ya upotevu wa mapato.

Queen aliongeza kuwa, suala la kupaisha uchumi katika kata zao ni kutoa hamasa kwa wananchi kuchangia huduma za kijamii na kuomba risiti wakati wanaponunua bidhaa kutoka madukani na gulioni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.