Matukio 23 ya utoroshaji madini yaripotiwa

Uhuru - - Habari - NA THEODOS MGOMBA, DODOMA

MATUKIO 23 ya utoroshaji wa madini hapa nchini yameripotiwa katika kipindi cha Julai 2015 hadi agosti 2016.

Hayo yalisemwa na Kaimu Kamishna wa Madini nchini,Ally Samaje, alipokuwa akitoa taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya wizara hiyo jana.

Samaje alisema madini hayo yaliyotoroshwa, yana uzito wa gramu 32, 813,21 na karati 572.84.

Alisema madini hayo yana thamani ya Dola za Marekani 1,505,477.68, na karati za sh. 151,338,373.84.

Samaje alisema baada ya kufanyika kwa marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010, kifungu cha 6 (4), hivi sasa kamishna wa madini amepewa madaraka ya kutaifisha madini yanayokamatwa.

Alisema mara baada ya madini hayo kutaifishwa, yatauzwa kwa njia ya minada.

“Baada ya marekebisho hayo, kamishna akishakamata madini kama hayana leseni au yametoroshwa, atayauza katika minada na fedha kuingizwa serikalini,íí alisema.

Alisema tayari madini yameshauzwa katika minada miwili, ikiwemo wa Arusha, uliofanyika mwaka 2014, ambapo serikali ilipata sh. bilioni 73, na mwingine mwaka huu, ambapo serikali ilipata sh. bilioni 1.3.

Wakichangia taarifa hiyo, wajumbe wa kamati kwa nyakati tofauti walihoji sekta hiyo kushindwa kuchangia fedha nyingi katika pato la taifa.

Mmoja wa wajumbe hao, John Heche, alisema inashangaza kuona katika baadhi ya migodi, kuna viwanja vya ndege, jambo ambalo linarahisisha kutoroshwa kwa madini hayo.

Alisema hana uhakika kama kuna mtu wa serikali, ambaye anaratibu ndege hizo, ambazo zinaingia kubeba madini moja kwa moja katika migodi, hivyo kuitaka serikali kuweka utaratibu huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.