Kinondoni yaongoza ukatili wa wanawake

Uhuru - - Habari - NA JACQUELINE MASSANO

KITUO cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC), kimesema takwimu zinaonyesha kuwa wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa vitendo vya ukatili kwa wanawake.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mratibu wa WLAC, Abia Richard, alipokuwa akizungumza kwenye semina ya mafunzo kwa wanamabadiliko wapya kutoka wilaya ya Ilala, iliyofanyika katika ukumbi wa Blue Pearls, Dar es Salaam.

Abia alisema utafiti unaonyesha kuwa, Kinondoni inaongoza kwa kuwa na vitendo vya ukatili kwa wanawake, ikifuatiwa na Temeke na Ilala.

Hata hivyo, aliziomba jamii kukemea vikali vitendo vya ukatili kwa wanawake vinavyoendelea nchini, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za unyanyasaji huo polisi.

Alisema asilimia kubwa ya wanawake wanaofanyiwa ukatili huo, hawakuwahi kumwambia mtu yeyote kwa sababu waliona ni jambo la kawaida katika maisha.

Aidha, alisema wanawake wengi, hasa wale waliofiwa na waume zao, wanafanyiwa vitendo vya kikatili, ikiwa ni pamoja na kunyangíanywa mali na kudhalilishwa mbele ya jamii.

“Wanawake wengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili, lakini wanaogopa kutoa taarifa polisi au kwenye vyombo vya serikali vinavyowazunguka kwa kuhofia maisha yao,”alisema.

WLAC, katika kampeni zake hizo zinazodhaminiwa na Taasisi ya Kitamaifa ya Oxfam, imefanikiwa kuelimisha wanamabadiliko 16,665, kutoka Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mogo ulioko kata ya Kipawa, George Mtambalike, alisema kwenye maeneo mengi nchini, viwango vya ukatili kwa wanawake na watoto vipo juu sana.

“Kwenye mtaa wangu, napokea kesi na malalamiko mengi ya ukatili, ambayo mengine hayajafika polisi na mengine yamefika, lakini bado olisi imeyafumbia macho,” alisema.

Hata hivyo, aliishauri WLAC na taasisi nyingine zinazopiga vita ukatili kwa wanawake, kujitahidi kuyaingiza masuala hayo kwenye mitaala ya shule ili watoto waweze kuelewa suala hilo tangu wakiwa wadogo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.