Watoto 1,940 wanaishi mitaani Mwanza

Uhuru - - Habari - NA MWANDISHI WETU

WATOTO 1,940, sawa na ongezeko la asilimia 25, wamebainika kuishi au kufanya kazi mitaani katika Jiji la Mwanza.

Aidha, imebainika kuwa katika miezi 12, idadi ya wasichana wanaofanya biashara ya ngono imeongezeka kwa asilimia 229, huku ongezeko kubwa likiwa ni la wasichana wenye umri kati ya miaka 11-14.

Hayo Peter Kent, ambaye ni Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Raily Children, wakati akitoa matokeo ya utafiti yaliyofanywa na shirika hilo katika Jiji la Mwanza.

Alisema katika utafiti huo, wamebaini kwamba watoto ambao hukumbwa na vitendo vya ukatilii katika umri mdogo, mara nyingi husababisha mzunguko wa umasikini kuwa katika hatari zaidi na matokeo hasi ya maisha.

Kent alisema matokeo ya utafiti huo pia yamebaini kuwa, idadi ya wasichana wanaofanya biashara ya ngono ni 418, kati yao 218 ni wenye umri chini ya miaka 18.

Hata hivyo, alisema utafiti huo umeonyesha kuwa, kumekuwepo na upungufu kwa asilimia 40, ya watoto wa mitaani wenye umri kati ya miaka 0-14, kwa kipindi cha miaka mitatu.

Alisema shirika hilo linatambua juhudi za serikali ya Tanzania katika kutoa huduma, msaada na ulinzi kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Kent alisema miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na serikali ni pamoja na kuwepo kwa Mpango wa Taifa wa Kukomesha Ukatilii dhidi ya Wanawake na Watoto, ambavyo vinaonyesha dhamira ya kweli ya serikali katika kukabiliana na watoto wa mitaani.

Alisema kutokana na ushirikiano wa karibu na serikali, wanaweza kuandaa kongamano la kimataifa la kusaidia harakati nchini na kuendeleza ufumbuzi katika huduma ya watoto wanaoishi mitaani.

Kent alisema shirika hilo linaandaa kongamano la kimataifa litakalofahamika kama ‘Kuvunja Mzunguko’, ambalo litafanyika mwezi ujao, mjini Dar es Salaam.

Alisema kongamano hilo litatoa fursa kwa wajumbe zaidi ya 250, kushiriki, kujifunza na kupata uelewa wa mkakati iliyothibitika ya kuvunja mzunguko wa ukatilii kwa familia dhidi ya watoto.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.