Kutoona kusiwafanye mpoteze vipajiDC Felix

Uhuru - - Habari - NA MARIAM MZIWANDA

yalibainishwa jana na MKUU wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, amesema matatizo ya kutoona isiwe sababu ya kumfanya mtu apoteze kipaji au uwezo wa kufanya kazi.

Lyaniva, alisema hayo juzi, jijini Dar es Salaam, wakati wa mafunzo ya ushonaji kwa watu wasioona, yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kushirikiana mkufunzi, Abdallah Nyangalio, ambaye ni fundi nguo asiyeona.

Alisema hatua ya TANTRADE kwa kushirikiana na Nyangalio, kutoa mafunzo hayo ni chachu kwa watu wasioona kutumia fursa hiyo kujifunza, kwani kuwa mtu usiyeona, siyo sababu ya kupoteza kipaji na uwezo wa kufanya kazi katika kujitafutia kipato.

Alisema watu hao wasioona waliopata fursa, ni vyema kutumia mafunzo hayo kuonyesha kuwa wanaweza kujiajiri binafsi na

kujitegemea, kujikimu na kuinua uchumi wa taifa kupitia ujuzi wa ushonaji.

“Nimefurahishwa na mafunzo haya ya ushonaji yaliyolenga kuwasaidia wenye ulemavu wa macho wenye ujuzi katika fani ya ushonaji. Ni tendo la kizalendo na naahidi kutoa cherehani kwa mwanafunzi anayeongoza katika mafunzo haya ya ushonaji baada ya kufuzu,”alisema.

Aliwaomba wanafunzi hao kuwa na nidhamu na kufuata maelekezo ya mwalimu vizuri ili waweze kufaulu na kunufaika na mafunzo hayo.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Abdallah Nyangalio, alisema yatawasaidia watu wasioona kuwa na ujuzi wa kushona, hatua itakayowaondoa katika dhana au kasumba ya wao kuwa ombaomba nchini.

“Nina uwezo wa kufunza watu 10, wasioona, lakini nazidi kusisitiza watokee wadau mbalimbali kusaidia kuendeleza juhudi hizi za kuchangia ununuaji wa vyerehani kwa wanafunzi waliodhamiria kujifunza, ili baada ya kuhitimu mafunzo haya, waweze kuendeleza ujuzi na elimu yao kwa watu wengine na kuwa na taifa la watu wengi wasioona wanaoweza kujitafutia kipato,” alisema.

Nyangalio alitoa shukrani kwa uongozi wa TANTRADE kwa kuratibu mafunzo hayo na kufanyia kazi maombi yao ya vifaa na cherehani, walizopatiwa kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Edwin Rutageruka, alisema mafunzo hayo ni ya kipekee, yatakayowasaidia watu wasioona kujiajiri, kujikimu katika mahitaji yao binafsi na pia kuchangia pato la taifa.

“TANTRADE imejipanga kuona bidhaa za nguo zitasaidia sekta ya viwanda nchini, hivyo tukiwaendeleza watu wenye ulemavu wa macho, wataweza kupata soko la ndani, ukanda wa Afrika Mashariki na baadae bidhaa zao kufika soko la kimataifa,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.