Mwijage avitaka viwanda kutumia falsafa ya ‘Kaizen’

Uhuru - - Habari - NA SIMON NYALOBI

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amevitaka viwanda kutumia falsafa ya Kaizen ili kuboresha uzalishaji wa bidhaa zao.

Mwijage, alitoa wito huo Dar es Salaam, jana, wakati wa utoaji wa tozo za pili za wakufunzi na kampuni zilizofanya vizuri katika utumiaji wa falsafa hiyo na kuongeza ufanisi.

Chimbuko la falsafa ya ‘Kaizen’ ni kutoka katika nchi ya Japan, ambayo inalenga kuongeza uzalishaji huku ikileta faida maradufu kwa wafanyakazi kwa mazingira ya kazi na usalama wao.

Mwijage alivishauri viwanda na kampuni nchini kuanza kujiandikisha na kuomba kupewa mafunzo ya falsafa hiyo ili ilete mabadiliko katika uzalishaji wao.

“Inabidi mtumie ‘Kaizen’ kwa sababu ni njia muhimu kuelekea katika maendeleo ya viwanda na mchango wake katika uchumi wa nchi,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka wazalishaji wa bidhaa nchini kuzingatia viwango na ubora wa bidhaa katika uzalishaji wao na kuhakikisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linakagua bidhaa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Adelhem Meru, alisema serikali itakuwa bega kwa bega na serikali ya Japan kuhakikisha mafunzo ya falsafa hiyo yanafanikiwa.

Dk. Meru alisema serikali imeridhika na manufaa ya utumiaji wa falsafa hiyo, hivyo kutaka iendelee kutumika katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi.

Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Toshio Nagase, alishauri serikali kuitumia falsafa ya Kaizen katika kufanikisha mpango wake wa kukuza viwanda ili kufikia maendeleo ya kiuchumi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.