Wafanyabiashara Arusha wamfagilia Rais Magufuli

Uhuru - - Habari -

WAFANYABIASHARA wakubwa wa mkoani Arusha wamempongeza Rais Dk. John Magufuli, kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi cha mwaka mwaka mmoja cha uongozi wake, kutokana na uadilifu na kupiga vita matumizi mabaya ya fedha za umma.

Pongezi hizo zilitolewa jana, jijini hapa na wafanyabiashara hao, wakati wa mkutano wao na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, uliofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, lengo likiwa kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.

Mmoja wa wafanyabishara hao, aliyejitambulisha kwa jina la Nicholaus Duhia, alisema mwaka mmoja wa Rais Dk. Magufuli umekwenda vizuri katika kusimamia ulipaji kodi, kurudisha heshima ya uadilifu serikalini na kupiga vita ufisadi na matumuzi mabaya ya fedha za umma, zilizokuwa zikitumika holela bila ya kuwepo na utaratibu maalumu.

Duhia, ambaye ni wakili, mkaguzi wa hesabu na ushauri wa kodi wa Kampuni ya Tax Plan Associates, alisema hakuna anayeweza kubisha kuwa hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kumuomba Rais Magufuli kurekebisha mabaya yote yaliyokuwa yakifanyika huko nyuma.

Alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Magufuli katika kipindi chake cha mwaka wa pili, kurudisha imani kwa wafanyabiashara wa hapa nchini ili waweze kufanya kazi bila ya woga.

Naye Sailesh Pandit, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Lodhia Group Enterprises & Signature Germ, alisema mbali ya kumkubali Rais Magufuli kwa utendaji kazi wake mzuri na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu’, heshima ya kazi serikalini imerejeshwa na imeimarika na watendaji wa serikali wanachapa kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, wakihofia kutumbuliwa endapo watafanya vibaya.

Pandit, alisema zipo kasoro chache, ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwake kusambaza mabomba ya plastiki.

“Mkuu wa mkoa naomba uingilie kati suala hili ili tuweze kufanya biashara hiyo na kutoa ajira kwa vijana wengi zaidi. Bila kulifanyia kazi kwa haraka jambo hili, viwanda vingi mkoani hapa vitafungwa na azma ya Rais Magufuli ya kutaka kuifanya Tanzania iwe ya viwanda haitatimia,”alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kiwanda chake kiko kwa zaidi ya miaka sita na kimeingia katika ushindani wa zabuni ya kusambaza mabomba katika mamlaka za maji Arusha, lakini kazi hizo zimekuwa zikipewa kampuni za Dar es Salaam, hali inayowafanya wakate tamaa.

Kwa upande wao, wafanyabiashara Willbroad Chambulu wa Kibo Safari na Atul Nittal wa Mount Meru Millers, walisema serikali ya awamu ya tano iangalie namna ya kupunguza utitiri wa kodi kwa wafanyabiasha wakubwa.

Akijibu hoja hizo, Gambo aliwahakikishiwa wafanyabiashara hao kuwa serikali yao itakuwa imara, kuwalinda na kuwasaidia pale watakapokwama, lengo likiwa ni kutaka wafanye kazi kwa ufanisi bila ya kipingamizi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.