Ofisa ardhi apewa siku 10 kueleza vilipo viwanja

Uhuru - - Habari -

MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, amempa siku 10 Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Anna Muamba, kueleza vilipo viwanja vya kijiji cha Sing’isi wilayani Arumeru.

Alitoa agizo hilo juzi, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya kipindi cha mwaka mmoja, kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM katika Wilaya ya Meru.

Mnyeti, alifikia hatua hiyo kutokana na mmoja wa wajumbe hao kutoka eneo hilo la Sing’isi, kueleza kuwa viwanja vya kijiji hicho vimeuzwa kwa watu binafsi bila ya uongozi wa kijiji kupewa taarifa.

Alisema awali, viwanja hivyo vilikuwa 92, lakini mpaka sasa vimebaki 56 pekee, hali ambayo inawashangaza wananchi wa kijiji hicho.

“Ninakupa siku 10, ofisa ardhi ulete maelezo ya kina juu ya viwanja hivyo, ambavyo vinalalamikiwa na wananchi wa Sing’isi,”aliagiza Mnyeti.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa UWT Wilaya ya Meru, Frida Kaaya, ambaye awamu iliyopita alikuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri, alisema vipo viwanja vingi, ambavyo madiwani waliviacha na ambavyo ni mali ya halmashauri, lakini anahofu kuwa vitakuwa vimeuzwa kinyemela na idara ya ardhi.

“Mkuu wa wilaya, halmashauri yote kwa sasa ni ya CHADEMA, hakuna diwani wa zamani, wote ni wapya. Mkurugenzi naye ni mgeni na wewe mkuu wa wilaya, hivyo watendaji wa idara ya ardhi wanafurahia jambo hilo kwa kuwa hakuna anayevifahamu,” alisema Frida.

Akitoa mfano, alisema katika eneo la Burka, lenye viwanja vya kijiji, vitengwa viwanja vitatu kwa ajili ya kumfidia mwananchi, ambaye alitoa eneo la soko la ndizi, lakini mpaka sasa mwananchi huyo hajapewa kiwanja hicho na alishafariki dunia.

Pia, alisema Kampuni ya Kabale Real Estate, ilikuwa inadaiwa viwanja vitatu katika eneo la Tengeru, wilayani humo, ambavyo mpaka sasa fedha za viwanja hivyo hazijaingia kwenye akaunti ya halmashauri.

Kwa upande wake, Mchumi wa CCM Wilaya ya Meru, Danielson Pallangyo, alisema watoto wa marehemu aliyetoa eneo hilo la soko, wamekuwa wakiomba CCM mara kwa mara kuwasaidia kupata viwanja hivyo vya fidia.

“Watoto wa marehemu wamekuwa wakija ofisini kwangu kama mchumi kudai viwanja. Nimeandika barua halmashauri kwa ofisa ardhi kuomba familia hii ipewe viwanja vyao, ambavyo vilitengwa na baraza la madiwani lililopita, lakini mpaka sasa hawajapewa. Naomba uisaidie familia hii ipate haki yao,”alisema.

Kufuatia hoja hizo, Mnyeti alimtaka ofisa ardhi huyo kutoa taarifa ya viwanja vyote vya halmsahauri hiyo na maeneo ya wazi ya umma kwani hawezi kuvumilia kuonawatu wachache wakichezea mali ya umma.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.