W Vikwazo vinavyokatiza ndoto za elimu kwa watoto wakike

Uhuru - - Elimu Na Utamaduni - NA SIMON NYALOBI

ATOTO wa kike ni sehemu ya idadi ya watu waliopo katika makundi mbalimbali nchini. Kwa mujibu wa Takwimu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto wa kike kati ya umri wa miaka 0-17, hapa nchini ni 11,263,891.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 48.8 ya watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 17, ambapo Tanzania Bara kuna watoto wa kike 10,943,846 na Tanzania Visiwani idadi yake ni 320,045.

Mwaka 2011, Umoja wa Mataifa (UN) ulipitisha kila ifikapo Oktoba 11, kila mwaka, kuwa siku ya mtoto wa kike duniani, ambapo mwaka huo, ilianza kuadhimishwa rasmi.

Mwanzoni mwa wiki hii, kulifanyika maadhimisho ya siku hiyo ikiwa ni miaka mitano tangu kuanzishwa kwake na mataifa mbalimbali duniani yaliadhimisha.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, suala la elimu kwa watoto wa kike lilipewa uzito wa aina yake, ambao wadau wa elimu walitaka kundi hilo lipewe haki hiyo ya msingi.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga, anasema jamii inatakiwa kuhakikisha inawapa elimu watoto wa kike ambayo ni haki yao ya msingi.

Sihaba anasema, watoto wengi wa kike wanakosa haki ya kupata elimu kwa sababu wanaozeshwa wakiwa na umri mdogo.

Anasema watoto wa kike wanaondolewa shuleni wakiwa chini ya umri wa miaka 18 na kwamba, hali hiyo ni kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kupata elimu.

Anawataka wadau na mashirika kuendelea kuwaelimisha wazazi na walezi wenye tabia ya kuwaozesha wanafunzi wakiwa shuleni.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo- Bisimba, anasema kituo hicho kinaungana na wadau wote duniani kuadhimisha siku hiyo ikiwa ni kutambua haki ya watoto wa kike ya kupata elimu.

“Katika familia nyingi za Kitanzania, mtoto wa kike anakosa fursa ya kupata elimu ukilinganisha na mtoto wa kiume na katika mazingira mengine wazazi wamediriki hata kuwaozesha watoto wao kwa ajili ya kupata fedha ya kusomesha watoto wa kiume, anasema.

Anaongeza kuwa, “Inasikitisha kuona mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto nyingi na cha kusikitisha zaidi mtoto huyu anaanza kubaguliwa kuanzia katika ngazi ya familia.”

Dk. Helen anasema ni ukweli usiofichika kuwa idadi ya wasichana wanaoshindwa kumaliza masomo kwa sababu za kupata mimba imekuwa ikiongezeka.

Lakini taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaopata mimba shuleni kutoka asilimia 23 hadi 26 hapa nchini.

Idadi hiyo inatafsiri kwamba, ni takribani ya watoto wa kike 8,000 Tanzania, kila mwaka, hukatisha masomo baada ya kupata ujauzito.

Aidha, idadi ya watoto wa kike ambao wanamaliza elimu ya msingi na kutopewa nafasi

Katika familia nyingi za Kitanzania, mtoto wa kike anakosa fursa ya kupata elimu ukilinganisha na mtoto wa kiume na katika mazingira mengine wazazi wamediriki hata kuwaozesha watoto wao kwa ajili ya kupata fedha ya kusomesha watoto wa kiume, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo watoto wa kike wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali zikiwemo kukatishwa masomo, kuozeshwa kwa lazima, ubakaji, ukeketaji pamoja na kutelekezwa, hivyo kushindwa kutimiza ndoto zake

ya kujiendeleza kielimu wanapokuwa wamefaulu au kutofaulu.

Hali hiyo inachangia wasichana kulazimishwa kuolewa wakiwa katika umri mdogo.

Hata hivyo, Dk. Hellen anasema kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wa kike kusafirishwa kutoka vijijini kwenda mjini kwa ajili ya kufanya kazi za ndani.

“Wapo watu wanawarubuni watoto wa kike kwa kuwachukua vijijini na kuwaleta mijini wakidai wanakuja kuwaendeleza kielimu, lakini matokeo yake baada ya kuwafikisha mijini wanawafanyisha kazi za ndani,” anasema.

Mkurugenzi huyo wa LHRC, anawaasa wazazi, walezi na viongozi wa serikali, kuhakikisha wanasimamia haki za watoto katika kupata elimu na kujiendeleza kimaisha.

“Tunaomba viongozi wetu katika ngazi zote za kijamii na hata kitaifa kuibeba ajenda ya haki za watoto na hususan haki za watoto wa kike kama ajenda ya kitaifa.

“Ili kuhakikisha wanalindwa dhidi ya vitendo viovu na wana mazingira salama ya kukua na kuwa watu wema na mustakabali mzuri wa maisha yao ya sasa na ya baadaye,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake(TAMWA) , Edda Sanga, anaupongeza Umoja wa Mataifa(UN), kwa kuanzisha siku hiyo muhimu ya mtoto wa kike, ambayo imelenga kuikumbusha jamii juu ya malezi bora ya mtoto wa jinsia hiyo.

Kwa mujibu wa Edda, watoto wa kike nchini wamekuwa wakikabiliwa na vikwazo vingi katika maisha yao, vinasababisha kukosa haki zao za msingi ikiwemo haki ya elimu.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo watoto wa kike wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali zikiwemo kukatishwa masomo, kuozeshwa kwa lazima, ubakaji, ukeketaji pamoja na kutelekezwa, hivyo kushindwa kutimiza ndoto zake,”anasema.

Edda anakumbushia utafiti wa UNICEF, uliofanyika mwaka 2009, unaonyesha kuwa wasichana wanne kati ya 10 walifanyiwa ukatili wa kijinsia kabla ya kutimiza miaka 18.

Vilevile, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 61 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 20-24, ambao hawakusoma na asilimia 39 ya wanawake wenye umri kama huo wenye elimu ya msingi tu waliolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18.

“Hali hii inafanya ndoa za utotoni kuwa ni sehemu ya ukatili kwa mtoto wa kike, TAMWA inaona kuwa, kuna umuhimu wa kuziangalia upya changamoto kisheria kwani zimekuwa kizingiti kwa mtoto wa kike katika kupata elimu,” anasema.

Vivyo hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, anawasisitiza wasichana kuwafichua wanaume waliowapa mimba ili wachukuliwe hatua kali za kisheria dhidi yao.

Zainabu anawaonya baadhi ya wanaume wenye tabia ya kupenda kuwashawishi wanafunzi kuwa na uhusiano nao wa kimapenzi, kuwa serikali imekaa chonjo kuwabaini.

Mkuu huyo wa Mkoa, anaunga mkono juhudi zinazofanywa na wmashirika na taasisi zinazoendesha mapambano dhidi ya mimba na ndoa za utotoni pamoja na kuwaelimisha walioathirika, hali ambayo inasaidia kutokomeza matatizo hayo.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalopinga mimba na ndoa za utotoni la Agape, Samwel Magina, anasema mpaka sasa waathirika wa mimba na ndoa za utotoni 117 na kuwapatia elimu ya masafa ya kidato cha kwanza, pili na tatu na wengine Chuo cha Maendeleo ya Jamii.

Mwenyekiti wa Baraza la Watoto mkoani Mwanza, Paulina Mashauri, anaiasa jamii kuacha kuwabagua watoto wa kike katika kuwapa fursa za elimu, ambayo ni haki yao ya msingi.

Paulina anasema kuwa, jamii inapaswa kubadili mtazamo wa kumuona mtoto wa kike kuwa hafai kupata elimu, kwani mawazo hayo yamepitwa na wakati katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake, Katibu wa baraza la watoto mkoani humo, Haleluya Benjamin, anaeleza kuwa watoto wa kike nchini wanakabiliwa na kikwazo vya kukosa elimu, hivyo jamii iwasaidie kuhakikisha hawakosi haki hiyo.

“Ni vyema sasa jamii ikaungana pamoja katika kutokomeza changamoto za watoto wa kike katika mimba za watoto wa kike wakiwa shuleni, tunaamini kuwa kwa ushirikiano huo, tutatokomeza tatizo hili,”anasema.

Vilevile, Msimamizi wa Baraza la Watoto, Karus Masinde, anaiangukia serikali na jamii kwa jumla, kuwapa kipaumbele watoto wa kike katika suala la elimu pamoja na fursa za uongozi ndani ya jamii.

Masinde anaeleza kuwa, watoto wa kike wakiwezeshwa katika elimu wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii katika nyanja za kiuchumi, hivyo kuleta maendeleo ya nchi.

Vikwazo hivi vinavyowakabili watoto wa kike, ambavyo vilielezwa na wadau katika elimu, vinapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee na serikali pamoja na jamii ili kuviondoa ndani ya jamii.

Ni vyema sasa jamii ikaungana pamoja katika kutokomeza changamoto za watoto wa kike katika mimba za watoto wa kike wakiwa shuleni, tunaamini kuwa kwa ushirikiano huo, tutatokomeza tatizo hili

WASICHANA wakiwa katika foleni ya kuchota maji, shughuli hii ni miongoni mwa sababu zinazowafanya washindwea kuhudhuria darasani na muda wa kujisomea.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.