Jiwe lenye taswira ya binadamu

Uhuru - - Elimu Na Utamaduni - NA DUSTAN NDUNGURU, RUVUMA

WILAYA ya Nyasa mkoani Ruvuma ni miongoni mwa wilaya zenye vivutio vingi vya utalii nchini, ambavyo vikitangazwa ipasavyo vinaweza kuliingizia taifa fedha za kigeni. Miongoni mwa vivutio hivyo ni pamoja na fukwe za asili ambazo hazifanani na fukwe zingine duniani ambazo zikiboreshwa zinaweza kuwavutia watalii wengi kwa wakati mmoja.

Vivutio hivyo, vimesahaulika kwa sababu havijafanyiwa utafiti wa kina ambao ungeweza kuvitambulisha ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi zikiwemo mbuga za wanyama pamoja na Mlima Kilimanjaro ambavyo vimekuwa vikiliingizia taifa mapato kupitia sekta ya utalii.

Wilaya ya Nyasa ni miongoni mwa wilaya zenye vivutio vingi vya utalii ambavyo vingeainishwa vingweza kulisaidia taifa kwa namna moja ama nyingine.

Hivyo kila Mtanzania ana jukumu kubwa la kuvitangaza vivutio hivyo ili viweze kuwavutia watalii wa ndani na nje kwenda kuvitembelea.

Moja ya vivutio vinavyopatikana katika wilaya hiyo ni jiwe la Pomonda lenye taswira ya binadamu, hadi kufika katika jiwe hilo itakulazimu usafiri kutoka Songea Mjini yaliyoko makao makuu ya mkoa wa Ruvuma kwa umbali wa takriban mita 300 ndani ya Ziwa Nyasa, kutoka Bandari ndogo ya Liuli na ni umbali wa zaidi ya kilometa 200.

Jiwe hilo Wajerumani waliliita Sphinxhaven kutokana na kuwa na vivutio lukuki vya utalii vilivyopo na muonekano wake wa taswira ya binadamu.

Utalii wa kihistoria ni aina ya kwanza ya utalii unaopatikana katika jiwe hilo, ambapo tangu vita vya kwanza vya dunia mwaka 1914 hadi 1918, pamoja na vita vya pili vya dunia mwaka 1939 hadi 1945, wakoloni wa Kijerumani na Wakiingereza walitumia pango kubwa lililopo katika jiwe hilo kama sehemu ya kujificha wakati wa mapambano.

Jiwe la Pomonda linaweza kuwahifadhi watu kati ya 200 hadi 250 na kwenye kilele chake kuna taa maalumu kubwa yenye rangi nyekundu ambayo ilikuwa ikitumiwa na nchi tatu za Tanzania, Malawi na Msumbiji.

Taa hiyo ilikuwa ikitumika wakati wa wakoloni wa Kijerumani, Kireno na Waingereza kama alama ya kuongozea meli katika ziwa Nyasa ili wasiweze kupotea wanapotaka kutia nanga kwenye Bandari ya Liuli.

Inaelezwa kuwa taa hiyo iliwawezesha kuiona Bandari ya Liuli, hata wakiwa katika nchi za Malawi na Msumbiji.

Kivutio kingine cha utalii ambacho kinapatikana katika eneo hilo ni mawe matatu makubwa ambayo wakazi wa eneo hilo wanaamini yamepangwa na Mwenyezi Mungu.

Mpangilio wa mawe hayo umekuwa ni kivutio na cha ajabu na ukifika katika eneo hilo utadhani limejengwa na mafundi ujenzi huku yakiwa yameacha njia maalumu ambayo inaweza kupitika kutokea upande wa pili hali inayowashangaza na kuwavutia wengi.

Jiwe hilo kihistoria pia ni sehemu muhimu ambayo inafaa kufanyia utalii wa kupiga mbizi, utalii wa kuruka kutoka juu ya jiwe hadi ziwani, umbali wa karibu mita 40.

Kutokana na vivutio lukuki vilivyopo katika jiwe hilo mara nyingi watalii kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakienda kufanya utalii na kujionea jiwe hilo la kihistoria.

Katika eneo lote linalozunguka jiwe la Pomonda kuna aina zaidi ya 120 ya samaki wa mapambo,hivyo mtalii anayefika katika jiwe hilo, kuna sehemu maalumu ambayo anaweza kufanya utalii wa kuvua samaki yeye mwenyewe.

Aidha, katika eneo hilo mtalii anaweza kupika au kupikiwa ugali wa asili wa muhongo ambao ni chakula maalumu kwa wakazi wa mwambao wa Ziwa Nyasa.

Jiwe la Pomonda ni eneo ambalo linafaa kwa ajili ya fukwe kwani kuna eneo lililofunikwa vizuri kwa mawe.

Mawe hayo yanamuwezesha mtu aliyepo eneo hilo kutoroa hata kama mvua inanyesha na pia kuna eneo maalumu ambalo linafaa kwa ajili ya kupiga picha.

Aidha, katika eneo la jiwe hilo mtu anaweza kuzunguka maeneo yote ya jiwe hilo kwa kutumia boti maalumu.

Hivyo basi, kutokana na jiwe hilo kuwa kivutio kikubwa cha utalii, wakati umefika sasa kwa watalaamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kutembelea eneo hilo la kihistoria ili waweze kufanya utafiti zaidi na kubaini vivutio vingine.

Serikali ya Mkoa wa Ruvuma, inasema vivutio vya utalii ambavyo vimetambuliwa katika mwambao wa Ziwa Nyasa vitaingizwa kwenye orodha ya vivutio vilivyopo mkoani humo na vitaendelezwa ili wananchi na serikali waweze kunufaika navyo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Isabela Chilumba, anasema mkakati wa wilaya hiyo ni kuhakikisha inaandaa mazingira mazuri yatakayowavutia watalii na wawekezaji mbalimbali ambao watatumia mandhari mzuri zinazoonekana fukweni mwa Ziwa Nyasa ikiwa ni pamoja na kujenga hoteli zenye hadhi.

Mbunge wa jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, anasema njia pekee ya kuvitangaza vivutio hivyo ni matangazo ya vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi.

Anasema hali hiyo itawezesha watalii wengi kufika katika eneo hilo kujionea urithi huo wa taifa.

JIWE la kihistoria la Pomonda ambalo lipo ndani ya Ziwa Nyasa, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

KIJANA akifanya utalii wa kuvua samaki wa mapambo ambao wanapatikana kwa wingi katika Jiwe la Pomonda lililopo ndani ya Ziwa Nyasa

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.