SMZ yajipanga kuinua na kuboresha sekta ya elimu

Uhuru - - Elimu Na Utamaduni - NA MWANDISHI WETU

ELIMU na mafunzo bora ni mkakati wa kipaumbele kufikia malengo ya mipango ya maendeleo yaliyowekwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika kufanikisha azma hiyo, Rais Dk. Ali Mohammed Shein, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta ya elimu inazidi kuimarika visiwani humo.

Pamoja na mikakati hiyo ya Dk. Shein, pia viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar nao wako bega kwa bega kutekeleza malengo ya serikali ya kuboresha na kutoa elimu bora.

Akizungumza katika kikao maalumu kati yake na uongozi wa Wizara ya Elimu mara baada ya kuwasilishwa kwa Ripoti ya Utekelezaji wa Kazi za Wizara hiyo kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, mwaka huu, Dk. Shein alisisitiza haja ya kujitegemea kwa kuwatumia wataalamu waliopo nchini.

Kikao hicho kilifanyika juzi, Ikulu Mjini Zanzibar, na kuhudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd na watendaji wa Wizara ya Elimu.

Dk. Shein pia alitumia fursa hiyo kuhimiza haja ya kutumia nyenzo na rasilimali zilizopo ili kupunguza gharama zisizo za lazima ili kuisaidia serikali.

Anasema kuna faida kubwa iwapo wataalamu waliopo kwenye wizara wakatumiwa vizuri, badala ya wataalamu kuwatumia kutoka nje ya nchi.

Dk. Shein anasema kwa upande wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imejaaliwa kuwa na wataalamu wa fani mbali mbali ambao wanaweza kuisaidia Wizara hiyo katika kufanya mambo yake.

“Wataalamu waliopo kwenye Wizara ya Elimu wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya elimu, hivyo kuna haja ya wataalamu hawa kutumika ipasavyo,” anasema.

Katika kikao hicho, Dk. Shein alieleza juhudi za makususdi zinazochukuliwa na serikali yake katika ukusanyaji wa mapato na kusisitiza azma ya kubana matumizi.

“Hakuna haja ya kujiwekea posho zisizokuwa na lazima ili fedha hizo ziweze kusaidia katika kuendeleza majukumu na mipango mengine ya serikali,” alisisitiza.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa wizara hiyo kwa kuwasilisha vyema mpango kazi na kuwataka viongozi na watendaji wa wizara hiyo kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili waendelee kupata mafanikio.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa uzalendo katika utekelezaji wa majukumu na kueleza kuwa suala zima la uzalendo litapewa kipaumbele mafanikio makubwa yanaweza kupatikana.

Kwa upande wake, Balozi Idd aliipongeza wizara hiyo na kusisitiza haja ya kuendelezwa vuguvugu la mashindano katika shule mbali mbali hapa nchini, ili kuweza kupata wanamichezo wazuri pamoja na kuongeza vipaji vya vijana katika sekta ya michezo.

Balozi Idd pia alitumia fursa hiyo kuihakikishia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuwa ataendelea kushirikiana na kuisaidia wizara hiyo ili kuweza kupatikana elimu iliyo bora hapa nchini.

Lakini Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, aliwataka watendaji wa wizara hiyo kuendelea kusimamia shule ili ziweze kufanya vizuri.

Aliwataka walimu wakuu na wasaidizi wao kushirikiana kwa pamoja katika kulifanyia kazi suala hilo ili elimu bora iliyokusudiwa iweze kupatikana.

Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, anasema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Wizara inaendelea na malengo ya kupanua upatikanaji wa huduma za elimu na kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.

Anasema Wizara imeweka vipaumbele katika kufikia dhamira ya utoaji wa elimu bora kwa wananchi wote na kuweza kupanga mipango mbali mbali ikiwemo kuimarisha elimu ya maandalizi.

Riziki pia anasema Wizara itaendelea na jitihada za kutayarisha na kuchapisha miongozo ya walimu, kuimarisha elimu ya msingi, sekondari, elimu mbadala na elimu ya watu wazima pamoja na kuimarisha elimu ya juu.

Anasema katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu, Wizara imetekeleza malengo mabli mbali yakiwemo matayarisho ya Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Elimu kwa kipindi cha miaka mitano (20162021).

“Mpango huo tayari umeanza hivyo ni imani yangu kwamba utakuwa na manufaa mapana kwa taifa na wananchi kwa ujumla,” anasema.

Riziki anasema ujenzi wa vituo viwili vya Mafunzo ya Amali vinavyo jengwa Makunduchi Unguja na Daya Pemba nao umeanza pamoja na ujenzi wa Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu kilichopo Mazizini ambao umekamilika.

Anaeleza kwamba Wizara imepokea madawati 5,150, viti 1,630 na meza 600, samani ambazo zilipokelewa kutoka kwa wabunge, wawakilishi na diaspora.

Pamoja na hayo alieleza kuwa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Utalii Maruhubi unaendelea na umefikia asilimia 20 ya ujenzi.

Waziri huyo pia anasema ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Karume nao unaendelea na umefikia asilimia 30, ambapo ujenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Amali Wingwi Mtemani nao unaendelea na umefikia asilimia

90.

RAIS Dk. Ali Mohammed Shein

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.