Taasisi za fedha zatakiwa kupanua wigo wa uwekezaji

Uhuru - - Habari - NA RACHEL KYALA

TAASISI zinazojishughulisha na fedha, hususani kwenye soko la mitaji na dhamana, zimetakiwa kupanua wigo wa uwekezaji ili kuinua kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa nchi.

Aidha, zimetakiwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili wapate uelewa juu ya uwekezaji wa soko la mitaji na dhamana kwa lengo la kuhamasisha uwekezeji kwa ajili ya maendeleo.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alitoa wito huo juzi, jijini Dr es Salaam, kwenye hafla ya utoaji tuzo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, waliofanya vizuri katika shindano la soko la mitaji na dhamana, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).

“Kasi ya ukuaji uchumi ya sasa, ambayo ni asilimia 7.2 kwa mwaka, inaweza kuongezeka iwapo mtachukua fedha zilizokaa bure kwenye akaunti za akiba na kuziweka katika soko la mitaji na dhamana,”alisema Dk. Ashatu.

Alisema wananchi wengi hawajui umuhimu wa masoko ya mitaji na dhamana, ndiyo maana fedha zao zimekaa bure kwenye akaunti, lakini iwapo watapewa elimu kupitia taasisi hizo, wataelewa na kuchukua hatua ili kukuza uchumi.

Aliitaka mamlaka hiyo kuwajengea uwezo na weledi wamiliki wa masoko hayo ili kuongeza tija katika utoaji huduma kwenye sekta hiyo.

Dk. Ashatu aliwataka watoa huduma hao kuwapatia nafasi za ajira wanafunzi waliofanya vizuri katika shindano hilo, pindi watakapohitimu masomo yao ili pia wapunguze gharama za usaili.

Licha ya changamoto nyingi kuainishwa na mamlaka hiyo, Naibu Waziri aliahidi kuwa, serikali itatoa ushirikiano kuzitatua, isipokuwa zile zisizo za kiutendaji.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nasama Massinda, aliiomba serikali kuwasaidia kuweka mazingira bora ili kuleta maendeleo katika sekta ya kukuza mitaji ili kuinua uchumi.

Alisema lengo la shindano hilo ni kutoa elimu juu ya fursa na faida ya kuwekeza katika masoko ya mitaji.

Washindi wanne wa awali walipatiwa sh.milioni 1.8, kila mmoja na kufuatiwa na washindi wanne waliojinyakulia sh. milioni 1.4 kila mmoja. Washindi wengine walizawadiwa sh. 500,000 kila mmoja na wanne wa mwisho sh. 200,000 kila mmoja.

Washindi 10, waliopata alama za juu, walipewa tiketi ya ndege kwenda nchini Ghana kwa mafunzo zaidi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.