Hukumu kesi ya Murunya kutolewa Novemba 25

Uhuru - - Habari - NA LILIAN JOEL, ARUSHA

KESI ya aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Bernad Murunya na wenzake watatu ya kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 66,890, inatarajiwa kutolewa hukumu Novemba 25, mwaka huu.

Kabla ya kupangwa kwa hukumu hiyo na Hakimu Patricia Kisinda,

anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha,

jana, alimaliza kusikiliza ushahidi uliotolewa na mshitakiwa wa tatu, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa NCAA wa wakati huo, Shad Kiambile na mshitakiwa wa nne, Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji wa Anga ya Cosmos, Salha Issa.

Katika ushahidi wake, Kiambile alidai mahakamani hapo kuwa, hakuna hasara waliyoisababishia serikali kwa kuwa fedha hiyo ilifidiwa kwa safari za watu wengine, japo yeye hakuwepo kazini kwani alikuwa amestaafu Januari, mwaka 2013.

Alidai anachokumbuka akiwa kazini, bosi wake Murunya, alimpa maelekezo ya kuandaa malipo ya safari ya aliyekuwa Waziri wa Utalii, Ezekiel Maige, msaidizi wake, Elgius Muyungi na Murunya mwenyewe na yeye alitekeleza kwa Meneja wa Idara ya Utalii.

Kiambile alidai Septemba 9, mwaka 2011, Kampuni ya Cosmos ililipwa Dola za Marekani 66,890, kwa ajili ya safari hiyo, japo hawakusafirisha watu kutokana na waziri kuikataa kampuni hiyo na kutaka asafiri kwa kampuni ya Antelope.

“Na hawa Antelope tuliwalipa Oktoba 29, baada ya kusafirisha abiria wetu na shirika halikuwa na shida kuzilipa kampuni hizo kabla au baada ya huduma,”alidai.

Pia, alidai kuwa katika ufungaji wa hesabu, haikuonyesha kama NCAA wana deni kwa Cosmos hadi alipoondoka, mpaka pale alipoelezwa wanadaiwa na ameshitakiwa.

Naye Mkurugenzi, Salha Issa, aliiomba mahakama hiyo imwachie huru kwa madai kuwa, kampuni yake haikula fedha hizo bali walifidia kwa watu watano na kwa kutumia ndege ya Emirates na KLM.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.