Majambazi wanane watiwa mbaroni Mwanza

Uhuru - - Habari - NA BLANDINA ARISTIDES, MWANZA

POLISI mkoani Mwanza inawashikilia watu wanane wanaosadikika kuwa ni majambazi kwa kufanya uhalifu katika matukio mawili tofauti jijini hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema watu hao wanahusika na unyangíanyi wa mali na wizi wa magari ndani na nje ya Mwanza.

Alisema katika tukio la ujambazi, polisi wamefanikiwa kukamata watu sita wakiwa na bunduki mbili za kienyeji zikiwa na risasi 23, ambazo zilikuwa zikifyatuliwa juu pindi wanapotaka kufanya unyangíanyi.

Kamanda Msangi alisema Oktoba 18, mwaka huu, saa saba mchana, katika kata ya Buswelu, wilaya ya Ilemela, askari wakiwa katika msako, walifanikiwa kuwakamata watu hao, ambao walivamia nyumba na kupora fedha taslimu sh.35,000 na mali ambazo hazijajulikana.

ìTuliowakamata ni Jeremiah Marigia (25), mkazi wa Singida, ambaye aliingia mkoani hapa kwa ajili ya kufanya uhalifu na tulipomuhoji, alikiri kufanya vitendo hivyo na kuwataja wenzake watano kuwa wanazo silaha wanazozitunza kwa mganga wa kienyeji, Benard Makayi, mkazi wa Ilemela,”alisema.

Alisema siku hiyo hiyo saa nane mchana, watu wawili, Rahim Feka (28) na Ally Kahalale (32), wakazi wa Dar es Salaam, walikamatwa wakiwa na gari la wizi lenye namba za usajili T 778 AZB Toyota Land Cruiser, lililoibwa Manispaa ya Ilala mkoani Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamanda Msani, watu hao walikuwa katika harakati za kutafuta wateja ili kuliuza jijini hapa.

Kamanda Msangi alisema gari hilo limepatikana Buzuruga, baada ya jeshi hilo kufanya upelelezi kutokana na taarifa walizozipokea kutoka Dar es Salaam, kuhusiana na kuibwa kwa gari hilo na huenda limeletwa Mwanza.

ìHawa watu bado tunaendelea kuwahoji, yawezekana wana mtandao unaofanya kazi za kuiba magari kutoka Mwanza na kuyauza Dar es Salaam au kuiba na kuyauza mikoa mingine. Wananchi wawe makini na vitu vya wizi kwa sababu gari haliuzwi kama bakuli mnadani,”alitahadharisha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.