Lukuvi atoa onyo kwa asasi za benki

Uhuru - - Habari -

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amezitahadharisha taasisi za kibenki kutokutoa mkopo kwa watu au taasisi kwa dhamana ya shamba ambalo litasababisha mgogoro ya ardhi.

Alitoa tahadhari hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, wakati akijibu hoja za wabunge baada ya serikali kuwasilisha taarifa ya ardhi kuhusu hatma ya matumizi ya mashamba makubwa yaliyotelekezwa.

Waziri huyo alisema mpaka sasa serikali imeshindwa kuyafutia hatimiliki mashamba pori ambayo hayajaendelezwa kutokana na kubainika kuwa, yamekopewa mabilioni ya fedha katika taasisi mbalimbali za kibenki hapa nchini.

Kutokana na hilo, alisema taasisi za kibenki nchini kama zisipokuwa makini kwa kutoa mkopo kupitia dhamana ya shamba na likaleta mgogoro kwa kutoendelezwa watakula nao sahani moja.

Alisema ni jukumu la serikali kuhakikisha linalinda umiliki halali kwa watu wenye hatimiliki na si kuwanyangíanya mashamba kiholela.

Lukuvi alisema kuwa, licha ya kuwa Rais amewapa jukumu la kuhakikisha wanafuta mashamba yote yasiyoendelezwa na kazi hiyo inaendelea, lakini wanahakikisha wanafuata sheria ili wasije wakashtakiwa.

Alisema wakati wanaendelea na utaratibu huo wa kufuta mashamba yasiyoendelezwa wamebaini kuwa, kuna mashamba mengi ambayo yana mikopo katika taasisi za benki hivyo lazima wafuate taratibu ili benki zisije kufilisika.

Waziri huyo alisema, katika mashamba hayo kuna yaliyochukuliwa mikopo nje ya nchi na yale yaliyochukuliwa mikopo ndani ya nchi na orodha yote wanayo wanaendelea kuifanyia kazi kikamilifu.

Alisema wakati taasisi hizo za kibenki zikijigamba kwa kushiriki katika sekta ya kilimo, zimekuwa zikishindwa kuangalia uhalisia ikiwa ni pamoja na kufika katika mashamba hayo kuona kama yanaendelezwa.

Lukuvi, alisema mkakati wa wizara hiyo hivi ni kukutana na taasisi za benki zote ambazo mashamba hayo yamekopea pesa ili waweze kufanya mazingumzo na kuona namna bora ya kumaliza mgogoro huo.

“Kimsingi mikopo yote iliyokopewa benki kupitia mashamba hayo, imesajiliwa kwa msajili hivyo hatuwezi kukurupuka lazima tufuate sheria katika kufuta mashamba hayo ili tusije kuingia kwenye matatizo na kubaki tukijilaumu,”alisema.

Alitolea mfano shamba moja ambalo limekopewa Dola za Milioni 16 mara nane, hivyo kusababisha ugumu wa kazi hiyo, na kwamba kuna ulazima wa kuwa makini.

Lukuvi alisema, kwa bahati mbaya licha ya mikopo hiyo kukopwa kwa dhamana ya mashamba lakini haitumiki kwa manufaa ya kuwekeza kwenye mashamba bali inatumika kuwekeza katika biashara nyingine ikiwemo kujenga nyumba za kupangisha nje ya nchi.

Alisema, endapo ingekuwa fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, sekta ya kilimo hapa nchi ingekuwa na mafanikio makubwa.

“Mashamba mengine ni vigumu kuyanyangíanya kutokana na hali hiyo,”alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Atashasta Nditiye, aliitaka serikali kufatilia na kutoa maelekezo ya namna mashamba hayo yanavyopaswa kutumika kwani kumekuwa na migogoro mingi katika miji mikubwa kutokana na wananchi kujichukulia sheria mikononi.

Pia, aliitaka serikali kutoa agizo la kisheria kwa kutoa mamlaka ya mipaka na ukubwa wa eneo ambalo wanapaswa kuhusika nalo watendaji wa vijiji kwani nao wamekuwa chanzo kikubwa cha migogoro.

Awali, Kamishna wa Ardhi Tanzania, Mary Makondo, wakati akiwasilisha taarifa ya matumizi ya mashamba makubwa, alisema kwa mujibu wa Sheria ya ardhi ya mwaka 1999, wizara iliagiza wakuu wote wa mikoa kuwasilisha taarifa za mashamba katika mikoa yao na hali ya maendelezo ya mashamba hayo.

Alisema kwa mujibu wa wakuu hao wa mikoa mashamba makubwa 1,912 yalihakikiwa na kati ya mashamba hayo 271 yalibainika kuwa yametelekezwa hali iliyosababisha wananchi kuyavamia na kufanyia shughuli mbalimbali.

Mary alisema, wizara hiyo imeanza kuchukua hatua kwa mashamba yaliyotelekezwa ambapo mkoani Morogoro pekee mashamba makubwa 12 yameripotiwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kibali cha kubadilishiwa matumizi.

Awali wakichangia taarifa huyo, Mbunge Mary Chatanda (CCM) aliiomba serikali kubadilisha matumizi ya shamba la kwa Mduru lililopo katika Halmashauri ya Korogwe mjini kutokana na mji huo kuingizwa katika mpango kabambe wa kuendelezwa.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, akijibu hoja hiyo, Halmashauri ya Korogwe inayopaswa kumwandikia notisi mwekezaji wa shamba hilo na kisha barua hiyo iwasilishwe wizarani ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.