Sekta ya madini sasa kuongeza pato la taifa

Uhuru - - Habari -

WAZIRI wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kufikia mwaka 2025 sekta ya madini inapaswa kuchangia asilimia 10 ya pato la taifa.

Profesa Muhongo alieleza hayo mjini hapa jana, wakati akitoa taarifa kuhusu shughuli za utafutaji madini na maendeleo ya sekta ya madini kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2015, sekta hiyo imechangia asilimia 4.3 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka 2014 kiasi ambacho bado ni kidogo.

Waziri huyo alitaja sababu zinazochangia kutoongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwa kiwango kikubwa kuwa ni pamoja na kushuka kwa bei ya madini kwenye soko la dunia na kutoanzishwa kwa migodi mingine mikubwa ya uchimbaji hivi karibuni.

“Kwa sasa uwezo wa uzalishaji wa dhahabu kwa migodi yote ni wakia milioni 1.25 kwa mwaka na uzalishaji kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 ni wakia milioni 5.68 sawa na tani 176.7 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 9.06 sawa na sh. trilioni 19.7,”alisema.

Profesa Muhongo alitaja mipango ya kuendeleza shughuli za madini nchini ikiwemo kuboresha ukusanyaji na usambazaji wa taarifa na takwimu za kijiosayansi, udhibiti wa utoroshwaji wa madini na ukaguzi katika shughuli za uzalishaji madini.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, alitaka kujua kuhusiana na utoroshaji wa madini unaofanyika katika baadhi ya migodi ikiwemo Mgodi wa ACCACIA ambao ndani ya mgodi kuna kiwanja cha ndege.

Akijibu swali hilo, Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje, alisema katika mgodi usafirishaji wa madini unafanyika kwa njia ya ndege kutokana na hatari ambayo inaweza kupatikana endapo dhahabu itasafirishwa kwa njia ya barabara.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.