Serikali yawashukia waajiri wanaokiuka sheria

Uhuru - - Habari -

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde, amewaagiza maofisa kazi nchini kusimamia sheria za kazi na kuwachukulia hatua stahiki waajiri wote ambao watabainika kukiuka sheria na kanuni za kazi.

Pia, amewataka wadau wa usafirishaji mkoani hapa kutumia fursa ya uwepo wa Makao Makuu ya Serikali, kuboresha huduma wanazotoa ili ziendane na hadhi ya makao makuu ya nchi.

Mavunde, alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, wakati akifungua mkutano wa utoaji elimu kwa wafanyakazi na wadau wa usafirishaji kwa njia ya barabara (TAROWU).

ìWakati huu ambapo serikali inahamia Dodoma waione kama fursa waache kufanya kazi kwa mazoea, kama una bajaji ifanye ifanane na mji mkuu, taksi nyingi ziko za muda mrefu tuzibadilishe tuendane na hadhi ya makao makuu,î alisema.

Alisema Dodoma imepokea neema ya kuwa makao makuu, hivyo kutakuwa na uhitaji mkubwa wa vyombo vya usafiri kutokana na ongezeko la watu.

Mavunde alisema pamoja na kushirikishwa kwa sekta binafsi kutoka nje na ndani ya mkoa wa Dodoma lakini wakazi wa mkoa huu wana nafasi kubwa.

Aliwasii kutumia vyema mafunzo hayo wanayopewa ili yawasaidie kujielimisha kwa kutambua fursa na kanuni kwa kuzingatia weledi katika utendaji.

Sambamba na hilo, Naibu waziri huyo aliwaagizaa maofisa kazi nchini kusimamia sheria za kazi na kuwachukulia hatua stahiki waajiri wote ambao watabainika kukiuka sheria na kanuni za kazi.

ìKumekuwa na changamoto mbalimbali katika sekta hiyo hali ambayo imekuwa ikisababisha malalamiko mengi ya waajiriwa kwa kuona waajiri hawatendi haki,îalisema.

Awali, Katibu wa TAROTWU, Salum Abdallah, alisema changamoto zilizopo katika sekta ya usafirishaji zimesababisha kila idara iwe ya majukumu yake ipasavyo hasa katika usimamizi wa haki, sheria na kanuni .

Abdallah, alisema kutotolewa kwa elimu juu ya sheria za kazi, kanuni na sheria mbalimbali zinazohusu sekta ya usafiri uchukuzi, imekuwa tatizo kubwa linalosababisha kuibuka malalamiko.

Naye, Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT) Zacharia Hanspope, alisema ni muhimu wafanyakazi wa sekta hiyo kutoa taarifa pindi wanapokutana na changamoto mbalimbali ili ziweze kufanyiwa kazi.

Rais huyo, aliahidi kutoa kompyuta na printa kwa ajili ya kusaidia kazi za ofisi za chama hicho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.