Watumishi ofisini

Uhuru - - Habari -

BAADHI ya watumishi wa serikali mkoani Mwanza, wanadaiwa kukimbia kazi kutokana na uhakiki wa vyeti unaloendelea kufanyika kwenye ofisi mbalimbali za umma.

Wakati watumishi wakikimbia ofisi zao, idadi ya wanafunzi hewa mkoani hapa inakadiriwa kufikia 11,000, huku Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiongoza.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Mwanza, juzi, alisema uhakiki wa vyeti unendelea mkoani hapa na kwamba hata yeye amehakikiwa.

“Kwa wiki mbili sasa baadhi ya watumishi wametokomea, hawapo kazini, wamekimbia uhakiki wa vyeti,”alisema Mongella bila kuwataja watumishi hao.

“Hata mimi nimehakikiwa, maana isifike mahali mkuu wa mkoa unafoka, kumbe huna sifa,”alisema.

Akizungumzia sakata la wanafunzi hewa, Mongella alisema wanakaribia kufika 11,000, huku Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikionekana kuongoza.

Alisema hatua za awali zilizochukuliwa ni kuwasimaisha kazi walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, zilizohusika na kuunda timu ya kuhakiki upya, ambayo imeanzia kazi Jiji la Mwanza, ambako tatizo hilo linaonekana kuwa kubwa zaidi.

Mongella alieleza kuwa, pamoja na kuwasimaisha walimu hao, bado kwa mujibu wa sheria ya sasa, wanaendelea kupokea mishahara hadi hapo uchunguzi utakapokamilika na kuchukuliwa hatua nyingine, kwani waliibia serikali kwa kuongeza majina ya wanafunzi hewa.

“Wenzetu hao (walimu) walitoa idadi kubwa kuliko waliyonayo ili kujipatia fedha nyingi,”alisema Mongella na kuongeza kuwa, uongozi wa Chama Cha Walimu (CWT) kutoka makao makuu, ulitarajiwa kuwasili Mwanza, jana, kuhusiana na sakata hilo la walimu wake.

Septemba, mwaka huu, walimu wakuu 62, wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza, walisimamishwa kazi baada ya kubainika wamesajili wanafunzi hewa 5,559 na kujipatia sh. milioni 132.5, kutokana na usajili huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, Agosti 20, mwaka huu, jiji hilo limebaini madudu hayo baada ya kuunda timu ya wataalamu waliofanya uhakiki katika shule 38, za sekondari na 78, za msingi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.