Viongozi wa mashina ya CCM kuhakikiwa Mwanza

Uhuru - - Habari -

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, kimeagiza wilaya zote kufanya uhakiki wa viongozi wake wa mashina (mabalozi), baada ya wilaya ya Sengerema kubaini kuwepo kwa mabalozi hewa 2,600.

Agizo hilo lilitolewa juzi, kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoani hapa, kilichofanyika kwenye ukumbi wa VETA, ulioko Nyakato.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Anthony Dialo, alisema ugonjwa wa ‘hewa’ hata ndani ya CCM upo, ambapo wilaya ya Sengerema imebaini kuwepo mabalozi hewa 2,600.

“Ugonjwa huu wa hewa ni hatari, hata CCM kuna mabalozi hewa. Sengerema kuna mabalozi hewa 2,600, hivyo tumeagiza kila wilaya ifanye uhakiki wa viongozi hao wa mashina,” alisema.

Katibu wa CCM wa wilaya ya Sengerema, Solomon Kasaba, alisema majina hewa ya mabalozi hao yaliongezwa na viongozi wasio waaminifu, kwa ajili ya kujipatia posho nyingi, lakini bahati nzuri waliyagundua kabla ya kuingizwa kwenye malipo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amekipongeza Chama Cha mapinduzi mkoani humo kwa kujenga mahusiano mazuri na watendaji wa serikali, ikiwa pamoja na kuwaalika kwenye vikao vya Chama.

Mongella alitoa pongezi hizo juzi, kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM na kuwaomba watendaji katika kila wilaya, kushirikiana na viongozi wa Chama katika ziara za kukagua miradi ya maendeleo ili wajionee utekelezaji wa Ilani unavyoendelea.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.