Dialo,Mhandisi Marwa wamtetea JPM

Uhuru - - Habari -

MENEJA wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Marwa Rubirya na Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Anthon Dialo, wamesema siyo sahihi kudai kuwa Rais Dk. John Magufuli hajaanza kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Dialo na Rubirya, walisema hayo juzi, kwa nyakati tofauti, kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Mwanza, kilichofanyika kwenye ukumbi wa VETA jijini hapa.

Walisema hayo baada ya baadhi ya wajumbe wa kikao hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu na Diwani wa Kata ya Nyanguge, Elisha Hilaly, kukiomba Chama Cha Mapinduzi, kimkumbushe Rais Magufuli ili atekelezea ahadi za barabara alizotoa wakati wa kampeni hizo.

{Barabara alizoahidi Rais, ambaye ni mwenyekiti wetu wa Chama, katika Kanda ya Ziwa ni nyingi, asipokumbushwa atasahau,” alidai Hilaly na kuongeza kuwa, ahadi hizo zikitekelezwa, CCM itatembea kifua mbele.

Akijibu hoja hiyo, Mhandisi Marwa alisema: ìSiyo sahihi kusema upande wa barabara, Rais hajaanza kutekeleza ahadi zake. Tuna changamoto ya fedha za makandarasi kuchelewa, lakini serikali ni sawa na familia, ukipanga fedha za kulipa ada, akija mkweo kavunjika mguu, itabidi umtibu.”

Alizitaja baadhi ya ahadi za barabara zilizoanza kutekelezwa kwa kiwango cha lami kuwa ni pamoja na ya Usagara-Kisesa, yenye urefu wa kilomita 17, ambayo ipo kwenye hatua za mwisho kukamilishwa.

Alisema barabara mpya ni Isandula Ngudu-Hungumalwa yenye urefu wa kilomita 71, Kamanga-Sengerema yenye urefu wa kilomita 36 na Daraja la Busisi Kigongo.

Nyingine ni Mwangwa Misasi, upanuzi wa barabara ya njia tatu ya Nyakato Buzuluga, Furahisha hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza na ujenzi wa daraja la juu la waenda kwa miguu Furahisha.

“Usagara- Kisesa, ujenzi ulisimama, lakini sasa unaendelea na mwishoni mwa mwaka huu utakamilika. Isandula- Ngudu hadi Hungumalwa, usanifu umeanza na Kamanga Sengerema taratibu za kandarasi zimeanza,” alieleza meneja huyo.

Aliongeza kuwa daraja la BusisiKigongo, utafiti umefanywa na kubaini karibu njia nzima mwamba uko umbali wa mita 10, isipokuwa kwenye mkondo wa mto, ambapo ni zaidi ya mita 50.

“Kwa sasa mhandisi mshauri anaendelea kuona nguzo zinazohitajika kupitisha daraja hilo zitakuwaje. Na kwa daraja la Furahisha, vifaa vyake vitatua bandarini Dar es salaam, Novemba 18, mwaka huu, ili tumalizie, lakini upanuzi wa Furahisha hadi Air Port na Nyakato-Buzuluga unaendelea,”alieleza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao hicho, Dialo alisema ahadi za Rais Dk. Magufuli, alizozitoa wakati akijinadi, ameanza kuzitekeleza na kuwaomba wajumbe wavute subira na kuondoa wasiwasi kuwa hazitatekelezeka.

Dialo alisema siyo kweli kuwa ahadi hizo hazitekelezeki na kuzitaja nyingine, ambazo utekelezaji wake umeanza kuwa ni pamoja na ujenzi wa meli mbili katika Ziwa Tanganyika na Victoria na kuupatia maji mji wa Magu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (MWAUWASA), Manyama Mecky, alikiambia kikao hicho kuwa, tenda ya mradi wa maji Magu utakaogharimu Euro mil. 15.3 (zaidi ya sh bl 13), imetangazwa.

KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Wilbroad Mutafungwa (wa tatu kulia), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Maendeleo, kilichopo Kata ya Kahe, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro. (Picha na Wilium Paul).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.