Yanga: Hapa Kazi Tu

Uhuru - - Michezo - NA ATHANAS KAZIGE, MWANZA

YANGA imeanza kazi baada ya kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi kusema kuwa wamebadili mfumo wa uchezaji wa kikosi chao na kuanzia sasa watakuwa wanatumia viungo wengi ili kupata ushindi.

Mwambusi, alisema hayo wakati akizungumza na gazeti hili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa juzi, akidai kuwa wamepania kutetea ubingwa na tayari wamebaini kasoro ambazo zilichangia kutoka sare na kupoteza mchezo dhidi ya Stand United.

Yanga ilifungwa bao 1-0 na Stand United mjini Shinyanga hivi karibuni na kutoka sare na timu za Simba na Azam jambo ambalo limewashtua benchi la ufundi na kuanza mbinu hiyo ya kutaka kuwatumia viungo wengi ili timu iweze kucheza kwa nguvu muda wote wa mchezo.

Alisema moja kati ya kasoro hizo ni kuhakikisha timu yao inacheza vizuri muda wote wa dakika 90 bila ya kuonyesha kuchoka kitu ambacho kitaweza kuwafanya washambuliaji kupata mipira mingi ya kufunga mabao na kuwapa furaha mashabiki wao.

“Kuanzia sasa, si umeona katika mchezo dhidi ya Toto tumetumia viungo wengi akiwemo Haruna Niyonzima ambaye kwenye mechi kadhaa hajacheza, pia wakati mwingine hata mabeki tutaboresha na kumpa kazi maalumu Nadir Haroub ‘Cannavaro,”alisema Mwambusi.

Alisema uamuzi wa kufanya hivyo kwanza utatokana na ugumu wa mchezo na hali ya uwanja kitu ambacho kwa sasa wamekitolea macho ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi zote zijazo.

Hadi sasa Yanga ipo nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo ikiwa nyuma ya timu za Stand United na kinara Simba ambayo ndio inaongoza ligi hiyo ambapo Mwambusi alisisitiza kuwa wana imani ubingwa bado ni wa Yanga.

Kauli hiyo, imekuja siku chache baada ya benchi zima la ufundi la timu hiyo kushushiwa lawama na wanachama na wapenzi wa timu hiyo kwenye mchezo dhidi ya Azam FC uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam hivi karibuni, baadhi ya wachezaji walionekana kuchoka hasa kipindi cha pili.

Kufutia hali hiyo, mashabiki hao walimtaka kocha, Hans Pluijm amtoe Juma Makapu kutokana na kile walichodai alionekana amechoka, lakini kocha huyo aligoma na hadi mwisho mchezo kati ya timu hiyo ulimalizika kwa suluhu.

Timu ya Yanga ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

WASANII nguli wa muziki wa dansi nchini, kutoka kushoto Roman Mng’ande, (Msondo Music Band), Mjusi Shemboza, Hassani Bitchuka na Abdallah Hemba (Sikinde), wakibadilishana mawazo, Dar es Salaam, jana baada ya mkutano kuhusu tamasha la kuchangia damu litakalofanyika Desemba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. (Picha na Christopher Lissa).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.