TOC kuchaguana Des. 10

Uhuru - - Michezo - NA AMINA ATHUMANI

UCHAGUZI Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), umepangwa kufanyika Desemba 10 mwaka huu mjini Dodoma.

Hatua ya TOC kupeleka uchaguzi huo mjini Dodoma ni kutokana na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk. John Magufuli kufanya mji huo kuwa Makao Makuu ya Serikali.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa katiba ya TOC, Ibara ya 20 (1).

Alisema fomu za kuwania uongozi TOC, zitaanza kutolewa Oktoba 25 mwaka huu na kurejeshwa Novemba 15 kwa mujibu wa katiba ya TOC ibara ya 23 (2) na zitapatikana ofisi za TOC Tanzania Bara na Zanzibar.

Bayi alisema nafasi zitakazowaniwa katika uchaguzi huo ni Rais, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina na Mweka Hazina Msaidizi.

Alisema katika nafasi hizo kuu fomu itakuwani sh. 200,000 huku nafasi za wajumbe wakinunua fomu hizo kwa sh. 150,000. Bayi alisema Novemba 18 kamisheni ya

uchaguzi itakutana jijini Dar es Salaam kupitia na kuzihakiki fomu kwa usaili wa wagombea utakaofanyika Novemba 22 kwa Tanzania Bara na Novemba 24, mwaka huu visiwani Zanzibar.

Bayi, mwanariadha mashuhuri Afrika, alisema kuwa Novemba 30, mwaka huu kamisheni ya uchaguzi itakutana kwa ajili ya kutangaza majina ya wagombea waliopita na waliokwama kwenye usaili huo.

Uchaguzi wa TOC, uitasimamiwa na kamisheni ya uchaguzi inayoundwa na Llyod Nchunga, Harrison Chaulo na Abdalah Mohamed walioteuliwa Agosti 27 mwaka huu kwa mujibu wa katiba ya TOC ibara ya 21 kipengele namba 6.

Mwanariadha huyo aliyewahi kutwaa medali ya dhahabu, alisema pia kutafanyika uchaguzi wa kamisheni ya wachezaji (KAWATA) utakaofanyika Desemba 6, mwaka huu siku nne kabla ya uchaguzi wa TOC.

KAWATA ipo chini ya ulezi wa TOC ambapo nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti, Katibu na Wajumbe wanne kwa idadi sawa ya jinsia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.