TASWA yawaita wadau wa

Uhuru - - Michezo - NA MWANDISHI WETU

KONGAMANO kuhusu mifumo ya kiuendeshaji ambayo klabu kongwe nchini za Simba na Yanga zinatarajiwa kufanyika kesho kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kongamano hilo limeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), likiwa na lengo la kupata maoni ya kitaalamu kuhusu mifumo hiyo.

Simba inatarajia kuingia mambo ya hisa na Yanga inapanga utaratibu wa kukodishwa na kongamano hilo litarushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Azam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando, alisema kuwa kongamano hilo halina nia ya kuzuia mabadiliko au kuharakisha mabadiliko katika klabu hizo.

Mhando, alisema badala yake litatumika kutoa elimu ya kutosha kwa wadau wa mpira wa miguu kuhusu mifumo hiyo na aina nyingine ya mifumo ya uendeshaji wa klabu duniani, hivyo itasaidia kujibu maswali mbalimbali ambayo pengine hayajibiwi kikamilifu.

Alisema kuwa baadhi ya mambo yatakayozungumziwa ni umuhimu wa mabadiliko katika klabu hizo, pia harakati za kuzibadili zilivyoanza miaka ya nyuma na matokeo yake na itazungumziwa pia mifumo ya uendeshaji ya klabu mbalimbali duniani.

Mhando alisema lengo ni kujadili kitaalamu bila ushabiki wa namna yoyote kwani nia ni kujenga na kuimarisha soka na wamealika wataalamu wa kada mbalimbali, viongozi wa zamani wa soka na baadhi ya wadau wa soka.

“Tunaomba mashabiki na wadau ambao hawakualikwa watambue tunathamini mawazo yao, lakini nafasi ya kuhudhuria ni chache wafuatilie kupitia vyombo vya habari,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.