Chirwa atangaza vita

Uhuru - - Michezo - NA ATHANAS KAZIGE, MWANZA

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Obrey Chirwa, amesema anashukuru Mungu kwa kumuwezesha kuanza kufunga mabao huku akitangaza vita na makipa.

Akizungumza kwenye juzi Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, mchezaji huyo alisema anashukuru Mungu kutokana na kuweza kufunga bao lake la pili dhidi ya timu ya Toto Africa.

Mchezaji huyo alifunga bao hilo katika mchezo kati ya timu hizo ukiwa ni wa Ligi Kuu msimu huu ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Bao jingine la Yanga lilifungwa na Simon Msuva ambapo Chirwa alisema siri kubwa ya kuanza kufunga mabao ni kuanza kuzoea mfumo wa uchezaji wa timu hiyo.

Mchezaji huyo raia wa Zambia, alisema kwamba mafanikio yake yametokana na kuwepo ushirikiano mzuri kati yake na wachezaji wenzake.

“Nina hakika sasa kazi yangu kubwa ni kufunga mabao, nitajitahidi kufunga mabao zaidi ili kuiwezesha Yanga kusaka ubingwa huku nikishirikiana vyema na wenzangu ndani ya dimba,”alisema Chirwa..

Hata hivyo, mchezaji huyo amesema kuanzia sasa ana kazi kubwa ya kuwafunga makipa kutokana na kuanza kuzoea mfumo wa ligi hiyo.

“Unajua toka ligi imeanza nilikuwa bado sijaanza kuzoea mchezo wa timu za Tanzania, sasa naanza kuzoea, nina imani nitafanya vizuri kama kocha ataendelea kunipanga na huku nikimuomba Mungu anipe afya njema,”aliongeza Chirwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.