Mnyama atafuna Mbao

Uhuru - - Michezo - NA AMINA ATHUMANI Simba: Mbao:

BAO la ‘usiku’ lililofungwa na mchezaji wa kiungo, Mzamiru Yassin, lilitosha kuipa timu ya Simba pointi tatu muhimu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mzamiru, aliwainua vitini mamia ya mashabiki wa Simba, baada ya kufunga bao pekee dakika ya 86 kwa shuti kali la mguu wa kulia. Simba ilishinda bao 1-0.

Timu ngeni ya Mbao kutoka Mbeya, ilicheza soka ya kutakata na kuibana Simba dakika zote 90 za mchezo huo licha ya kufungwa.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkali, baada ya Mbao kucheza kwa nguvu mchezo huo ulichezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba imefikisha pointi 26 na inaongoza katika msimamo wa ligi na Mbao imebakiwa na pointi 12 ikiwa nafasi ya nane. Timu ya Yanga ndio mabingwa watetezi wa kombe hilo.

Awali, mchezaji ghali raia wa Burundi, Laudit Mavugo, alishindwa kufunga bao dakika ya tatu, baada ya kupata pasi nzuri ya beki wa kulia, Janvier Bukungu.

Kocha Mcameroon Joseph Omog, alimpanga mchezaji huyo kwa mara ya kwanza, baada ya kusota benchi muda mrefu katika mechi zilizopita.

Dakika ya 10 Mavugo, alimuhadaa mwamuzi kwa kujiangusha ndani ya eneo la hatari la Mbao akitaka adhabu ya penalti kabla ya mabeki kuokoa hatari langoni mwao.

Kinara wa kufunga mabao wa timu ya Simba, Ibrahim Ajibu, aliitoka ngome ya Mbao dakika ya 17. lakini shuti lake lilitoka nje kidogo ya lango.

Ajibu, alipata fursa hiyo, baada ya kipa wa Mbao Emmanuel Mseja, kupangua shuti kali la Mavugo, akiwa ndani ya eneo la hatari.

Mbao ilijibu shambulio hilo dakika ya 22 baada ya nahodha, Hussein Sued, kuwapenya mabeki wa Simba, lakini alipiga shuti lililodakwa na kipa Vincent Angban.

Kiungo machachari wa pembeni wa Simba, Shiza Kichuya, nusura afunge bao baada ya mpira wake wa kona kumgonga kipa Mseja kabla ya mabeki kuokoa.

Dakika mbili baadaye, mshambuliaji wa pembeni wa Mbao, Dickson Ambudo, alishindwa kumalizia mpira na mabeki wa Simba waliokoa hatari miguuni mwake.

Simba iliingia kipindi cha pili kwa kumtoa Mavugo na nafasi yake kujazwa na Frederick Blagnon, kuongeza nguvu na dakika ya 46 Ajibu, alikosa bao baada ya mabeki kuokoa.

Mbao ilikosa bao dakika ya 48 baada ya mchezaji Pius Buswite, alijiangusha ndani ya eneo la hatari, lakini mwamuzi, Hans Mabena, alimshitukia.

Steven Kigocha wa Mbao, alikosa bao dakika ya 57, baada ya kufumua shuti kali umbali wa mita 18 kabla ya Blagnon kuweka wavuni bao la mkono ambalo lilikataliwa na mwamuzi Mabena dakika ya 60.

Mchezaji wa Mbao Frank Damas, alikosa bao dakika ya 71 baada ya kuwatoka mabeki wa Simba, lakini alitoa pasi fyongo iliyopotea.

Simba ilibisha hodi langoni mwa Mbao dakika ya 78 baada ya Blagnon, kukosa bao licha ya kuunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Mohammed Ibrahim, aliyeingia kujaza nafasi ya Ajibu.

Vincent Angban, Janvier Bukungu, Mohammed Hussein, Juurko Mursheed, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo/Frederick Blagnon, Ibrahim Ajibu/Mohammed Ibrahim na Mwinyi Kazimoto.

Emmanuel Mseja, Steven Mgaya, Steven Kigocha, Asante Kwasi, Pius Buswite, Yossouf Ndikumana, Hussein Sued/Frank Damas, Robert Magadula, Salmini Hoza, Emmanuel Mvunyekule, Dickson Ambudo.

BEKI wa timu ya Manchester United, Marcos Rojo, akiwasili kwenye Hoteli ya Lowry, muda mfupi kabla ya kupepetana na Fenerbahce ya Uturuki, katika mchezo wa Kombe la Europa uliochezwa jana usiku.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.