Carlos Kameni alicheza ligi ya juu enzi zake

Taifa Leo - - Front Page - NA CHRIS ADUNGO

IDRISS Carlos Kameni, 34, ni kipa mahiri mzawa wa Cameronn ambaye kwa sasa anakidakia kikosi cha Fenerbahce SK nchini Uturuki.

Kameni ametumia muda mrefu wa taaluma yake akiwajibika michumani mwa klabu ya Espanyol inayoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Hadi alipobanduka kambini mwa kikosi hicho mnamo 2012, alikuwa amechezeshwa katika jumla ya michuano 229 katika kipindi cha misimu minane.

Akiwa miongoni mwa wachezaji waliovalia jezi za Cameroon akiwa na umri mdogo zaidi, Kameni awajibishwa katika kikosi cha kwanza cha timu yake ya taifa akiwa na umri wa miaka 20 pekee. Tangu wakati huo, amekuwa sehemu ya kikosi cha Cameroon ambacho kimenogesha fainali mbili za Kombe la Dunia na fainali tano za Kombe la Afrika (AFCON).

Akiwa mzawa wa jiji la Douala, kipaji cha Kameni katika ulingo wa soka kilitambuliwa akiwa kitoto cha umri wa miaka 16. Kati ya 1995 na 2000, alipata fursa ya kudhihirisha ukubwa wa kiwango cha uwezo wake ugani akivalia jezi za kikosi cha Kadji Sports, Cameroon.

Aliingia katika mabuku ya historia mnamo 2000 kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kulinyanyulia taifa lake medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki.

Ufanisi huo ulimfungulia milango ya heri kambini mwa kikosi cha Le Havre AC nchini Ufaransa. Ingawa hivyo, alishindwa kabisa kukabiliana na viwango vikubwa vya ushindani kambini mwa klabu hiyo kiasi kwamba hakupata muda wa kupangwa katika kikosi cha kwanza.

Baada ya kusalia kuwa mchezaji wa akiba katika kipindi cha miaka minne cha kuhudumu kwake Le Havre waliomchezesha mara mbili pekee, Kameni alitumwa kwa mkopo kambini mwa AS Saintetienne kabla ya kisu cha makali yake kusenea hata zaidi.

Mnamo 2001, Kameni alianza kuhusishwa na uwezekano wa kujiunga na miamba wa soka ya Italia, Juventus japo matamanio yake yaliambulia pakavu.

Nusura Kameni afanikishe uhamisho wake hadi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kuvalia jezi za Wolverhampton Wanderers kwa mkopo wa mwaka mmoja mnamo 2003-04.

Hata hivyo, mpango huo uligonga mwamba baada ya kunyimwa kibali cha kufanyia kazi nchini

Uingereza.

Akiwa na umri wa miaka 20, Kameni alihamia RCD

Espanyol nchini Uhispania mnamo Julai

2004 kwa kima cha Sh600 milioni na akawa kipa nambari moja wa kikosi hicho katika mwaka wake wa pili.

Katika msimu wa 2005-06,

Kameni aliwasaidia waajiri wake kutia kapuni ufalme wa Copa del Rey, kipute kilichompa jukwaa mwafaka la kuwa msaidizi wa kipa Gorka Iraizoz aliyewajibishwa pakubwa katika mechi za La Liga.

Katika msimu uliofuata wa 2006-07, Kameni alishuhudia makali yake yalishuka pakubwa kiasi kwamba alipoteza nafasi yake katika takriban mapambano yote kwa mlinda-lango Iraizoz aliyewachochea Espanyol kuambulia nafasi ya pili katika kampeni za UEFA Cup.

Mapema 2006, Kameni alitepetea hata zaidi kiasi kwamba mashabiki waliotusi na kuanza kumbagua kwa misingi ya rangi yake walijipata wakifungulia mashtaka na kupigwa marufuku ya kuhudhuria mechi za Espanyol. Katika msimu wa 2008-09 ulioshuhudia Espanyol wakiburura mkia wa La Liga kwa kipindi kirefu, Kameni alijipata pabaya zaidi baada ya mwanzo kupigana na shabiki aliyemtusi mwishoni mwa kipindi cha mazoezi mnamo Januari 2008, kisha kupigana na mchezaji mwenzake, Gregory Beranger miezi minne baadaye.

Hata hivyo, Kameni bado aliwawajibikia waajiri wake katika jumla ya

mechi 37 kati ya 38 za msimu huo na mwishowe kuibuka kuwa nguzo muhimu zaidi kambini mwa Espanyol. Katika msimu huo, Kameni alivunja rekodi ya kipa mwenzake mzawa wa Cameroon, Thomas N’kono ambaye alikuwa amepiga jumla ya dakika 497 uwanjani bila ya kufungwa bao.

Baada ya kipindi cha misimu miwili zaidi akiwa akipangwa katika kikosi cha kwanza cha Espanyol, Kameni aliteremshwa daraja hadi kuwa kipa chaguo la tatu mnamo 2011-12 chini ya kocha wa mzawa wa Argentina, Mauricio Pochettino ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Tottenham Hotspur.

Mnamo Januari 13, 2012, Kameni alihamia kambini mwa Malaga CF na mchuano wake wa kwanza ni kibarua cha La Liga kilichowakutanisha na Espanyol mnamo Machi 25, 2012. Kipa huyo alitokea benchi katika kipindi cha pili kujaza pengo la Willy Caballero na kuwachochea waajiri wake kusajili ushindi wa 2-1 ugenini.

Baada ya Caballero kujiunga na Manchester City, Kameni alirejea tena kuwa chaguo la kwanza kambini mwa Malaga. Mnamo Septemba 26, 2015, aliyazuia makombora 31 aliyoelekezewa na wavamizi wa Real Madrid katika sare tasa walioisajili uwanjani Santiago Bernabeu. Kameni alitawazwa Mchezaji Bora wa mchuano huo.

Katika mechi iliyofuata, Kameni aliweka historia kwa kuwa kipa wa kwanza kuchangia bao katika La Liga baada ya kuwa chanzo cha mojawapo ya magoli yaliyofungwa na Charles katika ushindi wa 3-1 waliouvuna dhidi ya Real Sociedad

Mnamo Machi 2, 2016, Kameni alijifunga katika mechi iliyowashuhudia wakipepetwa 2-1 na Valencia mbele ya mashabiki wa nyumbani. Siku tatu baadaye, alilazimika kuondolewa mapema uwanjani baada ya kupata jeraha katika mechi iliyomalizika kwa 3-3 kati yao na Deportivo La Coruna.

Mnamo Novemba 19, 2016, alidhihirisha tena umahiri wake kwa kuwachochea waajiri wake kusajili sare tasa dhidi ya Barcelona.

Ilikuwa hadi Julai 2017 ambapo Kameni alisajili mkataba wa miaka mitatu na Fenerbahce. Kibarua chake cha kwanza katika kikosi hicho cha Uturuki ni mchuano uliowakutanisha na Alanyaspor mnamo Septemba 17, 2017 na kumalizika kwa wao kusajili ushindi wa 4-1.

Picha zote/hisani

Kipa mzawa wa Cameroon, Idriss Carlos Kameni ambaye kwa sasa anachezea kikosi cha Fenerbahce nchini Uturuki.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.